Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia
wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewaomba wananchi kuipigia
kura ya ndiyo katiba inayopendekezwa kwa kuwa ni bora na imezingatia
mahitaji ya makundi yote ya jamii.
Mama
Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa ombi
hilo jana wakati akiongea na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara
uliofanyika katika tawi la Mikumbi Magharibi kata ya Wailes wilayani
humo.
Alisema
katiba inayopendekezwa ni ya watanzania wote na imegusa maeneo yote
muhimu kwa ustawi wa wananchi, inazungumzia haki za wanawake, wazee,
wavuvi, watoto na watu wenye mahitaji maalum.
“Katiba
iliyopo sasa nayo ni bora, lakini hii inayopendekezwa ni bora zaidi
kwani imezitaja haki za mwanamke, mtoto, kijana,mzee na watu wenye
mahitaji maalum lakini katika katiba hii ya sasa makundi haya
hayatajwi. Msipoteze nafasi, siku ikifika jitokezeni kwa wingi
mkaipigie kura ya ndiyo”, Mama Kikwete alisema.
MNEC
huyo pia aliwahimiza wananchi hao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha
katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kuipigia kura katiba
inayopendekezwa na kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni
mwa mwaka huu wa kumchagua Diwani, Mbunge na Rais.
Alisisitiza,
“Zoezi hili la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura ni
jipya, hata kama unakitambulisho cha zamani ni lazima ukajiandikishe ili
uweze kupata kitambulisho kipya kwakuwa hicho cha zamani hakitatumika
tena”,.
Kuhusu
maambuki ya Virusi Vya Ukimwi alisema ni tatizo na kuwasihi wananchi
hao kujilinda na kutoruhusu ugonjwa huo usio na kinga wala tiba
kuingia ndani ya nyumba zao.
“Hali
ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi katika nchi yetu inazidi kupungua
kutoka asilimia 7.8 kwa mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 5.1 kwa mwaka
2014, hadi sasa jumla ya wananchi milioni 24 wamepima VVU kwa hiari.
“Kupima
kwa hiari kutakusaidia kujua kama unamaambukizi au la, na ikiwa utakuwa
na maambukizi utatumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa na
kuchukua tahadhari ili usiwaambukize wengine na kama hauna maambukizi
utajikinga”, Mama Kikwete alisema.
Akiwasalimia
wananchi waliohudhuria mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mwantumu
Mahiza aliwasisitiza wazazi na walezi kuona umuhimu wa kusimamia elimu
ya watoto wao kwani wakisoma wataweza kuzitumia fursa za kitaalam
zinazopo mkoani humo.
Alisema
hivi sasa shule za msingi na Sekondari ziko nyingi lakini cha
kushangaza kuna baadhi ya wazazi hawataki kuwapeka watoto wao shule.
Mahiza
alihimiza, “Kwa yeyote anayejijua ana mtoto nyumbani ambaye amefaulu
mtihani wa darasa la saba na hataki kumpeleka shule ajiandae kwakuwa
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake, natoa angalizo ifikapo
ijumaa ya wiki hii watoto hawa wawe shuleni kwani elimu ni mkombozi wa
maisha yao”, .
Katika mkutano huo wanachama wapya 202 walijiunga na Chama Cha Mapinduzi kati ya hao wawili walitoka Chama cha Wananchi CUF.
Wakati
huo huo MNEC Mama Kikwete alitembelea kwa nyakati tofauti matawi ya
Mmongo, Majani Mapana na Mikumbi Magharibi na kuongea na viongozi wa
Halmashauri kuu ya matawi mambo mbalimbali yahusuyo chama hicho .
Aliwataka
wajumbe kuwahimiza wananchi wawe na utamaduni wa kufuga kuku wa asili
(kienyeji) kwa kila kaya kwa kufanya hivyo itawasaidia kukuza uchumi
wao na familia zao na hivyo kujikomboa kutoka maisha ya umaskini.
Mama
Kikwete alisema ufugaji wa kuku wa asili hauna gharama kwani kuku
mwenyewe anajitafutia chakula, mfugaji atakachompa ni mtama au pumba
kidogo na maji ya kunywa pia nyama yake ni tamu na haina madhara kiafya
ukilinganisha na kuku wa kisasa.
Alisema,
“Ufugaji wa kuku una faida licha ya kuwa ni kitoweo bali pia ni
biashara, hivi sasa kuku mmoja anauzwa shilingi 12000 hadi 15000,
ukiuza mmoja ada ya shule itapatikana na mtoto atasoma na wewe mwenyewe
utavaa. Jitahidini kila kaya iwe na kuku japo 20”,.
Kwa
upande wa ardhi aliwasisitiza kutokubali kuuza maeneo yao kiholela
kwani maeneo mengi yako karibu na Bahari ya Hindi na thamani yake ni
kubwa hivyo basi wayatunze yatawasaidia katika siku zijazo .
Mama
Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za CCM ikiwa ni
pamoja na kufanya vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi ya mwaka 2010.CREDIT MICHUZI
Post a Comment