Shirika la afya duniani WHO pamoja
na wadau wake, mwishoni mwa wiki hii wanatarajia kuanza majaribio ya
ufanisi wa chanjo dhidi ya Ebola nchini Guinea.
Chanjo hiyo aina
ya VSV-EBOV imetengenezwa na wakala wa afya ya umma nchini Canada ambapo
imeelezwa chanjo nyingine ya pili itaanzishiwa majaribio kadri shehena
ya kutosha itakapo patikana.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt.Margaret
Chan amesema majaribio yatafanyika kwenye maeneo ya Basse Guinée ambayo
ndio yameathirika zaidi na Ebola kwa sasa nchini Guinea na utoaji wake
utaanzia kwa wagonjwa wapya na wale wote ambao wamekuwa karibu nao.
Lengo
la jaribio la sasa ni kutathmini iwapo chanjo hiyo itawapatia kinga
dhidi ya Ebola watu waliokuwa na makaribiano na mgonjwa na pili iwapo
utoaji wa chanjo utajenga kinga kwa wale waliopatiwa na hivyo kuzuia
maambukizi zaidi.
WHO imesema imejitahidi kwa dhati kuhamasisha
nchi zilizoathirika na ugonjwa huo pamoja na wadau ili kuendeleza mbinu
za kinga na iwapo chanjo hiyo itafaa itakuwa ni hatua ya kwanza ya kinga
dhidi ya Ebola.
Wadau wanaoshirikiana na WHO kwenye majaribio
hayo ya chanjo ni pamoja na wizara ya afya ya Guinea, madaktari wasio na
mipaka, MSF na taasisi ya afya ya umma, Norway.BBC
Post a Comment