Wnaharakati wa upinzani nchini
Burundi wanaandamana kwa siku ya pili wakipinga uamuzi wa kumtangaza
Rais Pierre Nkurunziza kugombea nafasi ya urais kwa muhula wa tatu.
Polisi walivunja maandamano kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha.
Watu
wapatao watatu waliuawa katika ghasi hizo nchini Burundi Jumapili
wakati polisi walipofyatua risasi za moto hewani kuwatawanya
waandamanaji.
Maelfu ya watu wamepuuza amri ya kuwataka kutokwenda kuandaamana mitaani katika mji mkuu Bujumbura.
Mwandishi wa BBC Maud Jullien
anaripoti kutoka katika mitaa ya Bujumbura kwamba watu walioshuhudia
matukio hayo wamemwaambia kuwa mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu
Pierre Claver Mbonimpa amekamatwa katika jengo la chama cha waandishi
wa habari nchini humo.
Awali alikitaka chama tawala kutomteua rais
kuwania awamu ya tatu ya uongozi, akisema kufanya hivyo ni kukiuka
katiba na mkataba wa amani wa Arusha.
Bwana Nkurunziza ametumikia
nafasi ya urais kwa vipindi viwili, akiingia madarakani baada ya
kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katiba ya Burundi
inamruhusu rais kuchaguliwa mara mbili. Lakini wafuasi wa Bwana
Nkurunziza wanasema anastahili kugombea kipindi kingine kwa kuwa
alichaguliwa na bunge mwaka 2005.
Upinzani unasema hatua hiyo
inatishia mpango wa amani ambao ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe
mwaka 2005 vilivyodumu kwa miaka 12.
Zaidi ya watu 300,000 waliuawa katika vita hivi.
Waandamanaji
wenye hasira Jumapili walirusha mawe na kuchoma matairi. Polisi
walijibu kwa kufyatua mabomu ya gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha
na kutumia risasi za moto, wakizuia maandamano kuingia katikati ya mji
mkuu Bujumbura.
Waandamanaji wengi wamekamatwa.
Polisi pia wanatishia kukifunga kituo cha redio binafsi kama hakitaacha kutangaza moja kwa moja kuhusu maandamano hayo.
Rais Nkurunziza amesema katika uteuzi wake uliofanywa na mkutano maalum wa chama tawala:
"Ningependa
kumwonya kila mtu: Kwa yeyote anayetaka kusababisha matatizo na chama
tawala kilichochaguliwa na watu, atajikuta kwenye matatizo," Imeripoti
Reuters.
Post a Comment