Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza na waandishi wa Habari jijini Mbeya(Picha na David Nyembe wa Fahari News) |
Waandishi wa Habari wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu(Picha na David Nyembe wa Fahari News) |
SERIKALI
imeazimia kumaliza migogoro yote ambayo ipo kwa wananchi ambapo Wizara ya
maliasili na utalii imeanza kuihesabu ili itatuliwe mapema iwezekanavyo ikiwa
ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha mapinduzi(CCM).
Hayo
yalibainishwa na, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alipokuwa
akizungumza na vyombo vya habari baada ya kumaliza ziara yake wilayani Mbarali,
ambapo alisema Serikali imeona ianze upya kufuatilia suala hilo ikiwa ni pamoja
na kutatua mgogoro uliopo.
Waziri
Nyalandu alilazimika kufanya ziara Wilayani Mbarali kufuatia kuwepo kwa mgogoro
wa wananchi wa vijiji 21 kugomea kupisha hifadhi ya Ruaha.
Waziri
Nyalandu alisema uamuzi wa kuvihamisha vijiji hivyo ili kupanua hifadhi ya
Ruaha ulitokana na tangazo la Rais (GN28) la kuifanya eneo la Ihefu na vijiji
vinavyoizunguka kuwa sehemu ya hifadhi.
Amesema
mgogoro huo ulianza mwaka 2009/2010 baina ya Usangu game reserve na bonde la
Ihefu kwenda Ruaha ambapo wakazi wa maeneo hayo ambao walipangwa kuhama
walitengewa fidia shilingi Bilion 4 na baadaye kuongezwa Bilion 3 na kuwalipa
fidia jumla ya Bilion 7.
Amesema
baada ya hapo mgogoro ulitokea kwa baadhi ya wananchi kudai kulipwa tofauti na
makadirio, wengine kudhurumiwa kabisa hivyo Serikali imeona wananchi hao
wasiondoke kwanza hadi madai yao yahakikiwe kwanza ambapo madai yote
yanatarajiwa kuanza kulipwa Julai 1, mwaka huu.
Aliongeza
kuwa mgogoro huo umetokana na tangazo la serikali kuandaliwa tofauti na matakwa
ya wananchi, pia maeneo yalioyoagizwa yakawa tofauti na maeneo
yaliyoorodheshwa ambapo maeneo ya awali hayakuguswa kabisa.
Waziri
Nyalandu alisema kutokana na hali hiyo, wananchi hao hawataondolewa katika
maeneo yao bali timu mbili zimeundwa ili kuchunguza sakata hilo.
Amesema
timu ya kwanza itafuatilia madai yote kisha watayapeleka kwa Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya ambaye atayawasilisha wizarani kwa ajili ya utekelezaji.
Amesema
timu ya pili itakuwa ya wataalamu wa Ikolojia ambao wataangalia mfumo wote wa
ekolojia na maji na namna ya kutatua mgogoro ili wananchi wawe sehemu ya
hifadhi pamoja na kuangalia namna maji yasiharibu mto Ruaha Mkuu.
Aidha
alitoa wito kwa Wananchi kuacha kuingiza mifugo yao ndani ya hifadhi ya Ruaha
mkuu bali wanapaswa nao kuwa sehemu ya uhifadhi.
Mwisho.
Post a Comment