Zaidi
ya asilimia 60 ya watoto wenye umri wa miaka 13 hadi 17 wanatumia zaidi
ya masaa mawili kila siku kuangalia mitandao ya kijamii pamoja na
vipindi mbalimbali vya Televisheni. Hii inaweza kuwa njia kubwa ya
kuunganisha, lakini pia kuna hatari zinazohusiana na kutumia muda mwingi
sana kwenye vyombo vya habari kijamii.
Leo
hii ni nadra kukuta familia ambazo watoto na vijana wake hawajaathirika
na vyombo vya habari na elektroniki kama vile televisheni, intaneti na
michezo mingine tofauti ya kompyuta.
Hata
hivyo utumiaji mkubwa na wa masaa mengi wa vyombo hivyo hauwahusu
watoto na vijana tu, bali watu wazima pia wameathirika na jambo hilo.
Kutokana
na sababu kadhaa za kimwili, kisaikolojia na kiroho, kuna udharura kwa
watoto kusimamiwa vyema na wazazi, mashirika na taasisi za kielimu na
kiutamaduni na kadhalika vyombo vya habari ili kupunguza madhara
yanayotokana na matumizi mabaya ya vyombo hivyo vya elektroniki. Licha
ya kompyuta kuwa na pande chanya tofauti za kimaendeleo, hasa katika
nyanja za kielimu na huduma za mawasiliano, lakini chombo hicho pia kina
nafasi hasi kwa watoto na hata kwa watu wazima.
Utumiwaji
usio na udhibiti wa chombo hicho na kadhalika vyombo vingine vya
elektroniki kama vile televisheni, unaweza kuyaweka hatarini maisha ya
watoto kutokana na athari zake mbaya kwa ustawi wa kiroho, kisaikolojia
na kijamii wa watoto hao.
Harakati
zetu za kifizikia na miamala yetu tofauti ya kijamii, ni umuhimu yenye
taathira kubwa kwa afya na tabia za mtoto. Kinyume chake, ikiwa mtoto
atatumia muda wake mwingi katika matumizi ya michezo ya kompyuta, basi
hawezi kunufaika na upande chanya wa kujenga akili yake wala harakati
bora kwa ajili ya kuufikia ukamilifu wake kijamii.
Mbali
na hayo, watoto pia wanaweza kukabiliwa na hatari ya kutekeleza vitendo
vya ukatili na visivyo vya kikatili hata katika umri wao mdogo. Hali
hiyo ambayo inaweza kufikiwa ghafla au hata kwa makusudi, huwaletea
watoto na vijana madhara yasiyoweza kufidika hasa kuhusiana na masuala
ya kiafya, kisaikolojia sambamba na kueneza kwa kiasi kikubwa matatizo
ya kimwili na kiakili kama vile utovu wa maadili, vitendo vya ukatili,
madawa ya kulevya, tabia mbaya katika jamii, kuzorota thamani za familia
na kuenea jinai na uhalifu wa kila aina katika jamii.
Ukweli
ni kwamba, wazazi hawajawachwa peke yao katika jukumu la kutoa malezi
bora kwa watoto wao, bali wataalamu wa mambo wamefanya utafiti wa kina
katika uwanja huo na kuwasaidia katika suala hilo kwa kuwasilisha njia
bora za malezi ambazo zinawavutia watoto na kuwafanya waishi maisha bora
katika jamii.
Watafiti
hao wanasema kuwa, licha ya kwamba haiwezekani kuwatenga watoto na
ulimwengu wa michezo ya kompyuta lakini tunaweza kuwaepusha na madhara
ya michezo hiyo kwa kutumia njia na mbinu zinazofaa.
Udhibiti
fulani wa matumizi ya kompyuta kila siku au kwa wiki, ni moja ya njia
hizo. Kwa mbinu hiyo, mtoto anaweza kutumia chombo hicho kwa muda na
kiwango kilichoainishwa na kila pale anapokwenda kinyume na kiwango
hicho, basi anapasa kuzuiwa na kuadhibiwa.
Hata
hivyo utumiaji mabavu na nguvu hauna nafasi katika hapa. Katika kesi
kama hiyo njia ya mazungumzo sanjari na kumzuia kwa muda, kutumia vitu
anavyovipenda mtoto huyo, inafaa kutumiwa hapa.
Wakati
mwingine mtoto hutumia vyema kompyuta kwa kujinufaisha kielimu na
chombo hicho muhimu cha teknolojia na kwa kweli katika hali kama hii
wazazi hawapaswi kumzuia mtoto kutumia chombo hicho cha kompyuta. Lakini
jambo linalopaswa kuzuiwa ni tabia ya mtoto huyo kutumia wakati wake
mwingi katika kichezo isiyofaa ya kompyuta.
Moja
ya nyenzo zingine za udhibiti ambazo zinaweza kutumiwa na wazazi katika
kusimamia mienendo ya mtoto, ni uwezekano wa kutumia mbinu
zinazodhibiti mfumo wa kompyuta. Kwa utaratibu huo watoto hawawezi
kuingiza program mpya au kuweka windozi tofauti ambazo ni rahisi kuweza
kuwaharibu watoto.
Njia
nyingine ni pamoja na kuzuia kuondolewa program zilizopo katika
kompyuta au kuzizuia zisifanye kazi, ni moja ya njia ambazo zinaweza
kutumiwa katika kuwadhibiti watoto.
Miongoni
mwa njia nyepesi zaidi kwa wazazi katika kumlinda mtoto wao wakati wa
kutumia njia na nyenzo zinazohusiana na ulimwengu wa intaneti, ni kuweka
mfumo wa kompyuta nje ya chumba chake cha kulala. Njia hiyo itawasaidia
wazazi wakati wa kutumia mtoto chombo hicho nao waweze kushuhudia na
kufuatilia kwa karibu michezo na shughuliza zote za mtoto huyo
anapotumia kompyuta.
Kwa
hakika vivutio vya kompyuta na michezo mingine ya kielektroniki kwa
watoto havina kikomo, na ikiwa hakutakuwepo usimamizi madhubuti wa
wazazi kwa mtoto wao, basi huenda mtoto bila kujijua, akatumia wakati
mwingi zaidi kuliko inavyotakiwa na hivyo kuathiri lishe, usingizi na
hata masomo yake.
Hapo
ndipo wazazi wanapotakiwa kuwa macho na kuhakikisha wanasimamia vyema
malezi ya mtoto wao sanjari na kumuandalia ratiba nzuri ya maisha yake
na kuchunga sheria watakazomuainishia kila wiki.
Aidha
wazazi wanatakiwa kumuweka mbali mtoto wao na ulimwengu wa elektroniki
na michezo ya kompyuta wakati wa kipindi cha masomo.
Watafiti
wanasema kuwa, kuna ulazima mkubwa wa kuzingatiwa wakati wa matumizi
ya watoto kwa vyombo vya umeme kama vile kompyuta, labtop na tablet na
kile ambacho kinahusiana na ulimwengu wa kielektroniki, kwani utafiti
unaonyesha kwamba matumizi mengi ya vyombo hivyo kupita kiasi na kufikia
kiwango cha uraibu, hupunguza uwezo wa kifikra wa mtoto.
Na kukithiri kwa maradhi
hayo kwa watoto ndio mwanzo wa kufeli katika hatua zao za kielimu
sanjari na kushindwa kukabiliana na mikikimikiki mingine ya kimaisha
ambayo anapaswa kukabiliana nayo katika mustakbali wa maisha yake ya
mbeleni.
Katika
matumizi ya michezo ya kompyuta au ulimwengu wa intaneti, kuna udharura
wa kujitenga na mambo machafu yasiyofaa. Aidha inaelezwa kuwa, kutumia
sana kompyuta na intaneti, taratibu huibua tatizo la unene, ambalo mara
nyingi hupelekea watoto na hasa vijana wengi kujichukia wenyewe kutokana
na tatizo hilo. Hivyo kuna haja kwa wazazi kuwaepusha watoto wao na
unene na uzembe unaosababishwa na matumizi ya muda mrefu ya vyombo vya
umeme hasa michezo ya kompyuta.
Wataalamu
wengi wanaamini kuwa, ni muhimu kuwatenga watoto walio na umri wa chini
ya miaka mitatu na aina yoyote ya matumizi ya kompyuta. Kwa maana
nyingine ni kwamba, umri huo hauoani na matumizi ya kompyuta au video.
Hata
hivyo ikiwa mtoto aliye na umri wa chini ya miaka mitano ataingia
katika ulimwengu wa matumizi ya vyombo hivyo na kuvizoea, basi lazima
awekewe sheria na vidhibiti maalumu vya kumuwezesha kukabiliana na
hatari ya ulimwengu huo. Kwanza anapasa kufahamishwa ni kwa kipindi gani
anatakiwa atumie vyombo hivyo na kisha baada ya hapo ajishughulishe na
kazi nyingine.
Watafiti
wanapendekeza kuwa, mtoto mwenye umri wa kuinukia anatakiwa atazame kwa
saa moja au masaa mawili filamu na katuni, upekuzi katika intaneti na
michezo mingine ya video katika kompyuta. Ikiwa mtoto kwa siku atatumia
dakika 45 kucheza mchezo wa kompyuta na muda mwingine mdogo kutazama
televisheni na mwingine mfupi kujishughulisha na harakati za kifizikia,
basi hakutakuwepo na wasi wasi wa kuathirika afya yake. Lakini ikiwa
atatumia masaa mengi kujishughulisha na michezo ya kompyuta zaidi ya
kiwango kinachotakiwa, basi hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili
kukabiliana na hali hiyo.
Madaktari
wanashauri kwamba, watoto wanatakiwa kutumia masaa mawili tu kwa siku
kutazama televisheni. Televisheni ina athari nyingi muhimu kwa watoto
wengi wanaosoma na hasa katika kupumzisha mwili na fikra zao.
Hivyo
wazazi na walimu wanatakiwa kusimamia ni kiasi gani watoto wanapaswa
kutazama televisheni. Hii ni katika hali ambayo katika miaka ya awali
watoto wanaosoma shule za msingi, huwa hawana uwezo wa kupanga vyema
ratiba za kutazama televisheni.
Makala
haya yameandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari na Afisa
Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
anapatikana kwa barua pepe; sawebenjamin@gmail.com.credit Michuzi Matukio
Post a Comment