Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Betty Pentzel na mwenzake Maryam Salim na kutoka Popatlal Sekondari, Tanga wakimuelekeza Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, kuhusu utafiti wao wa ‘The Effects Of Chemical Hair Products And Its Solution’. 

Tunu Ngajilo kutoka Mbeya Sekondari akimuelekeza Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, kuhusu utafiti wao wa Automatic Irrigation System ambao uliwafanya washinde tuzo tatu.


Na Daniel Mbega wa brotherdanny.com
KWA Geofrey Ndunguru na Yusuph Mwenda, wanafunzi wasioona kutoka Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea, kushinda Tuzo Maalum ya Sayansi ya Spicenet mwaka huu 2015 ilikuwa ni faraja ambayo kamwe hawakuiota.
Na hawakuiota kwa sababu hata ushiriki wao ulikuwa kama bahati nyingine ambayo hawakuitarajia kutokana na ukweli kwamba wanafunzi wengi wenye ulemavu wamekuwa wakiachwa nyuma katika mambo mbalimbali, achilia mbali kushiriki maonyesho ya sayansi kama ilivyotokea kwao mwaka huu.
“Ushindi wa tuzo hii kwetu sisi ni faraja kubwa sana kwa sababu tunadhani kilio chetu kimesikika na kuna watu wanaotambua kwamba kumbe hata sisi tunahitaji na tunastahili kujifunza sayansi kama kwa wale wanaoona, tunawapongeza sana waandaaji wa maonyesho haya,” alisema Yussuph Mwenda mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Alhamisi Agosti 6, 2015.
Wanafunzi hao walikuwa miongoni mwa wanafunzi 240 walioshiriki maonyesho ya sayansi ya mwaka 2015 kati ya Agosti 5-7, 2015 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam na andiko lililowapa ushindi ni Analysis of Blind Students Attitude Towards Science (Uchambuzi wa Hulka ya Wanafunzi Wasioona Katika Mwelekeo wa Sayansi).
Mwenda alisema tuzo hiyo ni ushindi kwa wanafunzi wote wenye ulemavu wa aina mbalimbali, na akaiomba serikali na jamii kutowabagua kwani wanaweza kufanya vizuri kama wanafunzi wasio na ulemavu.
Taasisi ya kuibua vipaji vya sayansi na kuchochea watoto kuyapenda masomo ya sayansi ya Young Scientists Tanzania (YST) ambayo kila kwa mwaka wa tano sasa imekuwa kiandaa na kuratibu maonyesho hayo imeona kwamba kuna haja ya kuwashirikisha wanafunzi wote, bila kujali hali zao, ili washiriki na waipende sayansi kama inavyotakiwa.
Dk. Gosbert Kamugisha, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa YST, anasema wanashukuru kwamba maonyesho hayo yanazidi kupanuka kila mwaka na kushirikisha wanafunzi wengi bila kujali jinsia wala ulemavu.
“Ni mwaka wa tano sasa tunaendesha maonyesho haya, lakini kila mwaka yanazidi kupanuka, mwaka huu tumewashirikisha wanafunzi wengi zaidi, wakiwemo hawa wasioona ambao kwa kweli wanahitaji kujifunza sayansi japokuwa kuna changamoto kubwa hasa ya vifaa vya kujifunzia na kufundishia,” anasema Dk. Kamugisha.
Wakati taasisi hiyo inaanzishwa mwaka 2009, si Dk. Kamugisha wala mwanzilishi mwenza Joseph Clowry walioamini kwamba baada ya muda wangeweza kupata mwitikio kama unaoendelea kuonekana mwaka hadi mwaka.
Hiyo yote inatokana na ukweli kwamba, kwa miaka sasa masomo ya sayansi yamekuwa hayapewi kipaumbele sana na wanafunzi wengi kutokana sababu nyingi zikiwemo ukosefu wa walimu; vifaa vya kujifunzia na kufundishia; kutokuwepo mkazo wa vitendo kutoka serikalini (wizara husika) kupitia mitaala ya elimu na wanafunzi wengi kukosa mwamko wa kusoma masomo hayo.
“Hatukutegemea kuona mwitikio huu tunaouona leo, lakini naamini kwamba hizi ni dalili njema kabisa na zinatutia hamasa ya kuendelea kuibua vipaji kupitia maonyesho haya na kuwahamasisha walimu wa sayansi kuendelea kufundisha kwa bidii ili tupate wataalam wengi wa utafiti na ugunduzi pia,” anaongeza Dk. Kamugisha.
Anasema kwa kawaida timu ya YST huzunguka nchi nzima kutembelea shule mbalimbali ambazo zinaonyesha kufundisha masomo ya sayansi na kuwapa miongozo walimu pamoja na hamasa ya kufundisha masomo ya sayansi.
Pamoja na changamoto mbalimbali za kufifia kwa masomo ya sayansi nchini, lakini Dk. Kamugisha anasema kwamba bado Tanzania haijachelewa katika kuandaa kizazi cha wanasayansi na kwamba kinachotakiwa ni dhamira, uthubutu na jitihada, kwani taifa lolote linahitaji wanasayansi ili liweze kuendelea.
Mwanzilishi Mwenza wa YST, Joseph Clowry, anasema kuna dalili nzuri za mafanikio tangu walipopata wazo la kuanzisha taasisi hiyo mwaka 2009, kwani mwitikio umeonekana kuwa mkubwa kadiri miaka inavyokwenda.
“Ili taifa lolote liendelee, ni vyema kuwekeza zaidi katika tafiti za kisayansi kwa kuanzia kwenye ngazi za chini kabisa, kuwafanya watoto wapende udadisi wa kisayansi na kufundisha kwa bidii wawapo shuleni.
“Ireland ilikuwa nyuma kimaendeleo kama zilivyokuwa nchi nyingi ulimwenguni, lakini walipoamua kuwekeza kwenye sayansi hali imebailika hivi sasa ambapo wapo wanasayansi mahiri kabisa na vijana nao wanapenda kujifunza masomo ya sayansi,” anasema Clowry.
Makamu Rais wa BG Tanzania anayeshughulikia Sera na Masuala ya Uhusiano, John Ulanga, ambao ndio wadhamini wakuu wa maonyesho ya mwaka 2015, anasema wameamua kujitolea kudhamini YST kwa sababu wanatambua kwamba Tanzania inahitaji kuwa na wanasayansi wengi hasa linapokuja suala la mafuta na gesi ambayo yakitafitiwa yakapatikana na kuchakatwa yanaweza kuinua uchumi wa taifa kwa kiwango kikubwa.
“Tunahitaji wanasayansi wa kutosha katika sekta hii adhimu ya mafuta na gesi, tukiwa nao wazalendo itakuwa ni bora zaidi, hivyo ni lazima tuwadhamini watu kama YST ambao wanajenga msingi imara katika kuwapata wataalamu wa kesho,” anasema Ulanga na kuongeza kwamba mwaka huu kampuni yake imetoa Dola 200,000 (takriban Shs. 450 milioni) kwa ajili ya udhamini wa maonyesho hayo na akaahidi kwamba mwakani watatoa kiwango kama hicho au zaidi ili kufanikisha.
Fionnuala Gilsenan, Balozi wa Ireland nchini, anasema kwamba alikuwepo nchini Tanzania kama mtafiti kwa miaka sita, aliporejea kwao ndipo akateuliwa kuwa Balozi nchini Tanzania, hivyo anayafahamu mazingira ya Tanzania pamoja na suala zima la elimu ya sayansi.
“Ninayajua mazingira, lakini kwa kweli nawaunga mkono YST kwa maono yao ya kuwekeza kwenye sayansi kupitia maonyesho kama haya ambayo yanajenga msingi uliobomoka wa masomo ya sayansi, nchi yangu iko nao bega kwa bega kuwasaidia kwa kadiri itakavyowezekana,” anasema na kuongeza kwamba, Tanzania bado haijachelewa kuwekeza kwenye sayansi.
Na ili kuhakikisha wanafunzi wanayapenda masomo ya sayansi na kuyaelewa vizuri, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, wakati akifungua maonyesho hayo, akashauri walimu katika shule za msingi na sekondari kutumia lugha ya Kiswahili kufundisha sayansi, kwani lugha hiyo inaeleweka vizuri.
Alhaj Mwinyi alisema Kiswahili ni lugha ya taifa inayoeleweka na kila mmoja, hivyo sayansi ikifundishwa kwa lugha hiyo itasaidia zaidi watoto kuyapenda masomo hayo kwa kuwa hawatakuwa na hofu ya lugha ngeni ya Kiingereza inayotumika kwa sasa.
“Mimi wakati naingia darasa la tano, mwalimu wangu wa sayansi alikuwa raia wa Scotland, lakini alimfundisha sayansi kwa Kiswahili na ndio msingi wangu mkubwa wa kulifahamu vyema somo la sayansi,” anasema.
Maonyesho ya mwaka 2015, mbali ya kudhaminiwa na kampuni ya BG Tanzania na Ubalozi wa Ireland nchini kupitia Shirika la Msaada la Irish Aid, pia yalidhaminiwa na Songas, Read International, Solaris, Spicenet, Karimjee Jivanjee, Masumin Printways,  First Car Rental, Vernier, na Human Development Innovation Fund (HDIF).
Tangu maonyesho hayo yalipoanza mwaka 2011, mpaka sasa takriban wanafunzi 1,000 wameshiriki.
Washindi wa mwaka 2012 walikuwa Aisha Nduku, Monica Shinina na Nengai Moses kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibosho mkoani Kilimanjaro ambao walitafiti madhara ya mbolea za kemikali na nitrogen yanayopatikana kwenye mto jirani na shule yao. Andiko lao lilisema: Industrial fertilisers and increased nitrites in water.
Washindi wa mwaka 2014 walikuwa Dhariha Amour Ali na Salma Khalfan Omar kutoka Shule ya Sekondari Lumumba mjini Zanzibar kwaandiko lao la Changing Attitudes to control Flies in Tanzania, na washindi wa pili walikuwa Upendo Mwanuo na Josephine Chomya kutoka Shule ya Sekondari St. Christina's na andiko lao la The  Masai diet as a way of controlling diseases.
Mwaka 2015 washindi walikuwa Edwin Luguku na John Method wa Mzumbe Sekondari na andiko lao la ‘Reducing the use of plastic bags in Tanzania’, wakati washindi wa pili walikuwa Emmanuel Lemalali na Emmanuel Sanga kutoka Tanga Technical na utafiti wao wa ‘A Simple Method For Controlling Ecto-parasites’.
Washindi wa mwaka 2013 walikuwa Jafari Ndagula na Fidel Samwel kutoka shule ya sekondari Ilongero ya mkoani Singida kutokana na andiko lao la "A Drip Irrigation System using recycled materials" wakati washindi wa pili walikuwa mabinti kutoka Shule ya Sekondari Haile Selaissie ya Zanzibar ambao ni Shemsa Abdulkarim na Salha Jumbe Said ambao andiko lao lilikuwa "Analysis of Kupagawa and its causes".

(IMEANDALIWA NA www.brotherdanny.com. Simu 0656-331974)


Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top