Mwomba rufani, Dr. Devota John
Marwa, (Mrufani) ni msomi mbobezi katika taaluma ya michezo, akiwa ni mhadhiri
katika kitengo kinachojihusisha na taaluma ya michezo katika Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam. Akiamini kwamba anakidhi vigezo vilivyowekwa kwa nafasi ya mgombea
uenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake(TWFA), alichukua fomu ya kuomba
kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho.
Maombi hayo yalikumbana na pingamizi
zilizoletwa na wakereketwa wawili wa soka la Wanawake, Bi. Chichi Mwidege na
Bi. Mwajuma Noty, ambao kwa pamoja walimwekea pingamizi Mrufani, kwamba hakidhi
matakwa ya kanuni za ugombea wa nafasi ya Mwenyekiti.
Waleta mapingamizi walidai kuwa
Mrufani hakuwa na sifa zilizoainishwa katika Kanuni za Uchaguzi za T.F.F. (TFF
Electoral Code) Ibara ya 9 (tisa) kipengele cha 3 (tatu), kinachomtaka mgombea
awe amejihusisha na uongozi wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.
Aidha Ibara ya 28 (ishirini na nane)
kipengele cha 3 (tatu), kinamtaka mgombea awe amejihusisha japo miaka 2
(miwili) katika shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu nchini. Kamati ya Uchaguzi iliridhia mapingamizi hayo
na kuliondoa jina la Mrufani katika orodha ya wagombea wa nafasi hiyo ya
Mwenyekiti. Rufani hii ni matokeo ya uamuzi huo wa Kamati ya Uchaguzi
uliotolewa taraehe 22 Julai, 2015.
Kwa ujumla, sababu za kupinga
maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi zinaweza kuhesabiwa kuwa ni mbili. Moja ni
iliyojikita juu ya hitilafu katika kuamua kwamba Mrufani hakuwa na uzoefu
katika uongozi wa soka kwa muda ulioainishwa. Sabau nyingine ni kwamba Kamati
ya Uchaguzi illibua sababu ambayo haikuwa katika Hati ya pingamizi iliyoletwa
na Mleta pingamizi.
Wakati ambapo Mleta pingamizi alijikita katika
kipengele cha 28(3), Kamati iliibua kipengele cha 28(8), cha Katiba ya TWFA
kinachomtaka mgombea awe ametimiza uzoefu wa uongozi wa miaka mitano, ambacho
hakikuwemo katika hoja za pingamizi zilizowasilishwa na mleta pingamizi.
Katika kufikia uamuzi wake, Kamati
ya Rufani ilizipitia sababu za Mrufani kama zilivyoletwa, na baada ya
kusikiliza maelezo ya Mrufani na hoja za Mwakilishi wa TFF, Wakili Msomi Edward
Augustino, na imeamua kama ifuatavyo. Tutaanza na hoja ya mwisho.
Je, Kamati ilikuwa sahihi kuibua
kipengele ambacho hakikuletwa katika hati ya mapingamizi? Kamati inaweza kuibua
kipengele hicho endapo kwa kufanya hivyo, itakuwa imejielekeza katika nia njema
ya maslahi ya suala linalozungumziwa.
Sharti jingine ni kwamba hoja hiyo
inyoibuliwa isiwe na athari hasi(prejudicial) kwa mhusika. Kaika suala hili
hata hivyo, hoja iliyoletwa na Mleta pingamizi, yaani hoja chini ya kifungu cha
28 (3), imeainisha kipindi kifupi cha uzoefu
(miaka 2), na hoja iliyoibuliwa na
Kamati inahitaji uzoefu wa miaka 5.
Endapo Mrufani angekuwa na uzoefu wa
miaka 3 hadi 4, bado angekwama kutokana na hoja iliyoibuliwa na Kamati. Hii kwa
vyovyote ingekuwa ni athari hasi (negative impact) katika harakati za Mrufani.
Ni vema
Kamati zinazosikiliza malalamiko
zikajikita kwenye malalamiko yaliyoletwa na wahusika wenyewe. Kama pigamizi
lingekuwa liko juu ya kipengele hicho tu, tusingesita kukubaliana na sehemu hii
ya rufani. Hata hivyo, takwa la uzoefu wa miaka 5 limeainishwa pia katika Ibara
ya 9 (3), ambayo ilikuwa ni sehemu ya mapingamizi yaliyokuwepo kwenye hati ya
mapingamizi.
Kwa sababu hiyo, Kamati ya Rufani
haioni kama hoja hiyo ina mashiko. Haitaitilia maanani. Hoja kuu ndani ya rufaa
hii ni je, Kamati ya Uchaguzi ilijielekeza vema kuhusu suala la uzoefu wa
uongozi ulioainishwa na Katiba?
Mrufani ameieleza Kamati ya Rufani
mlolongo wa shughuli ambazo amekuwa akizifanya, nyingi zikiwa zimejikita zaidi
katika taaluma. Miongoni mwa shughuli hizo ni kuandaa Mpango Mkakati wa
kuendeleza soka la wanawake. Mpango huu uliridhiwa na kuwasilishwa Makao Makuu
ya Shirikisho la Mpira Duniani, yaani FIFA.
Maelezo mengine ni kushiriki katika
kuongoza timu mbali mbali kule Chuo Kikuu, zingine zikiwa za watoto wadogo
ambao baadhi ya matunda yake ni wachezaji walioibukia kwake kama vile Simon
Msuva. Alisema zaidi kuwa alishiriki kuandaa warsha ilizoandaliwa kwa
ushirikiano kati ya FIFA na TFF.
Aidha. Alisema kuwa amekuwa kiongozi
tangu akiwa bado kwenye vyuo vya ualimu, na baadaye alipohitimu na kufanya kazi
kama Mwalimu, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliko mpaka
sasa. Akasema, hata alipokuwa Sweden kwa masomo ya juu pia lijihusisha na
programu za maendeleo ya soka la wanawake.
Wakili msomi wa TFF akijibu hoja
hizo, alikubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi kuwa Mrufani hajaonesha
popote kwamba amewahi kuongoza soka, akasema Mrufani ni mtaalamu tu kama msomi,
jambo linaloweza kufanywa na msomi yoyote. Akamalizia kwa kuiomba Kamati ya
Rufani za Uchaguzi kuitupilia mbali rufaa ya Mrufani kwa kukosa mashiko.
Tofauti na Kamati ya Uchaguzi,
Kamati ya Rufani imeona kuwa kwa maslahi mapana ya mchezo wa soka katika ujumla
wake, ni vema kuweka tafsiri pana (wide interpretation) juu ya sifa
zinazozungumzwa, badala ya kuweka tafsiri finyu (restricted/narrow
interpretation) kama ilivyofanya Kamati ya Uchaguzi.
Baada ya kufanya hivyo, kuhusiana na
Mrufani, Kamati imeona kuwa ana sifa zinazostahili. Kupitia sababu alizozitoa,
na vielelezo vyake, Kamati ya Rufani haina wasiwasi kuwa Mrufani ana uzoefu
mbali mbali sio katika soka tu, bali pamoja na michezo katika ujumla wake.
Tumeshuhudia katika maelezo yake
kwetu kwamba ushiriki wake katika hatua mbali mbali, japo hakuwahi kuchaguliwa,
sio ushiriki wa kitaaluma tu, kama msomi mwingine yeyote. Ni ushiriki wenye
dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko/maendeleo katika soka la wanawake.
Maelezo
yake kuwa aliaandaa programu ya
maendeleo ya soka la wanawake, hayakupingwa. Kamati ya Uchaguzi ingeangalia
namna ambavyo “visheni” iliyomo katika programu ile ambavyo ingeweza
kutekelezwa na mtu aliyeaiandaa. Kwa hiyo, katika hoja hii, Kamati inakubaliana
kuwa Mrufani
anazo sifa stahiki, na kukatwa kwa
sababu hii, Kamati ya Uchaguzi haikujielekeza vema. Kwa hiyo, Mrufani ameshinda
rufaa yake? Kamati ya Rufani inachelea kujibu swali hili moja kwa moja.
Utaratibu wa kuwasilisha rufani ulikiukwa, na hapa ndipo rufaa hii inapokwaa
kisiki. Chini ya Ibara ya 13 (1) cha
Kanuni ya
Uchaguzi (Electoral Code), mgombea
ambaye hakuridhika na maamuzi, atawasilisha rufaa yake ndani ya siku 3 (tatu)
tangu uamuzi anaoupinga ulipotolewa.
Kipengele cha 3 (tatu) cha ibara
hiyo kinasema kwamba Mrufani yoyote atakuwa na uhalali endapo rufaa yake
imewasilishwa kwa mujibu wa kanuni hizo.
Uamuzi unaolalamikiwa ulitolewa tarehe 22 Julai 2015, sababu za rufaa
ziliandaliwa tarehe 27 Julai na sababu hizo za rufaa zililipiwa tarehe 28
Julai, 2015. Ni dhahiri kwamba rufaa ililetwa nje ya muda uliowekwa na kanuni,
na kwa hiyo inakosa uhalali kisheria na kikanuni.
Japo katika mwenedo na maamuzi yake
Kamati ya Rufani za Uchaguzi haifungwi na taratibu za kimahakama, suala la muda
wa kuwasilisha rufani sio miongoni mwa mambo ambayo Kamati inaweza
kutoyazingatia. Kwa sababu hiyo, Rufaa hii imetupwa, lakini kwa sababu tofauti
na zile za Kamati ya Uchaguzi.
Pamoja na uamuzi huu, Kamati ya
Rufani za Uchaguzi inapenda kwa namna ya kipekee kumpongeza Mrufani kwa
jitihada alizozionesha kutaka kuitumikia TWFA. Ni matumaini ya Kamati kuwa
hatokata tama, na kwamba atakuwa tayari, akitakiwa kufanya hivyo, kupitia
taalum yake, kushirikiana na wenzake katika jitihada za kuendeleza soka la
akina mama lililo na changamoto lukuki.
Imetolewa na,
JULIUS M. LUGAZIYA
Mwenyekiti-Kamati ya Rufani za
Uchaguzi
Post a Comment