1. Chama cha ACT-Wazalendo kinasikitishwa sana na maujai yanayoendelea nchini Burundi na hasa Mji Mkuu wa nchi hiyo Bujumbura. Hali hii ya mauaji imesababishwa kwa kiasi kikubwa na uamuzi wa Rais wa sasa wa nchi hiyo Ndugu Piere Nkurunzinza kuendelea kugombea na hatimaye kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo katika mazingira yaliyovunja demokrasia na utawala bora.
2. Tangu machafuko nchini Burundi yaanze zaidi ya watu 100 wameshauawa kufikia wiki hii na wengine kadhaa kujeruhiwa. Aidha, wimbi la wakimbizi kutoka Burundi linarudi kwa kasi na wengi wao wakikimbilia nchini Tanzania.
3. Bahati mbaya sana Jumuiya ya Kimataifa na hasa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Burundi ni mwanachama, haikuchukua hatua za maana za kuzuia kuchafuka kwa utawala wa kidemokrasia na utawala wa sheria nchini Burundi, na wala haichukui hatua stahiki kuzuia mauaji yanayoendelea. Hii ni kinyume kabisa na Mkataba unaounda Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao unatoa kipaumbele cha juu kulinda uhai na haki za raia katika Jumuiya hiyo
4. Kutokana na hali ya kisiasa na usalama nchini Burundi, na kwa kuzingatia nafasi ya kihistoria ya Tanzania katika kutafuta na kufanikisha Mkataba wa Amani nchini Burundi, na kwa kuzingatia nafasi yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, tunaitaka serikali ya Tanzania, kwa hali kubwa ya dharura, ichukue hatua zifuatazo:
a. Iitake serikali ya Jamhuri ya Burundi kukomesha mara moja maujai yanayoendelea nchini humo na kuwahakikishia raia wa nchi hiyo usalama
b. Iitake serikali ya Jamhuri ya Burundi kuitisha mkutano wa wadau wote wa siasa na utawala nchini humo ili kujadili mustakabali wa nchi hiyo kisiasa na kijamii, ikiwemo uwezekano wa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayosimamia Katiba ya Burundi kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia
c. Itumie nafasi yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuitakaJumuiya hiyo kuzuia machafuko nchini Burundi na kuhakikisha kwamba utawala wa demokrasia na utawala wa sheria unazingatiwa nchini humo
5. Chama cha ACT-Wazalendo kinasisitiza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itakosa uhali wa kuendelea kuwepo kwake kama itaendelea kuwa Jumuiya ya viongozi wa nchi zinazounda Jumuiya hiyo na kishindwa kusimamia haki za kuishi na haki za kiraia za wananchi wa Afrika Mashariki.
Venance Msebo
Katibu wa Kamati ya Mambo ya Nje
ACT-Wazalendo
Jumatano, 16 Desemba 2015
Post a Comment