Na Krantz Mwantepele.
Tanzania
ya leo, imepitia mabadiliko mengi yanayogusa kila sekta tangu ilipojikomboa na
kuwa nchi huru baada miaka 53 ya utawala wa kikoloni.
Kwa
mfano, katika kipindi hicho hadi sasa, nchi imeshuhudia kuimarika kwa huduma
mbalimbali za kijamii. Kwa uchache, huduma hizi ni pamoja na afya, elimu, demokrasia, utalii, viwanda na
miundombinu mbalimbali.
Katika
sekta ya elimu, ongezeko kubwa la shule kuanzia ngazi ya awali hadi chuo kikuu
limeshuhudiwa. Hii ni moja ya hatua kubwa kuwahi kufikiwa tangu nchi ilipoanza
kujitawala. Katika sekta ya afya, hospitali, zahanati na vituo vya afya vimejengwa
kwa wingi kutegeme mahitaji ya watu.
Miundombinu
ya barabara imeimarika maradufu na kuifanya Tanzania kuongoza Afrika Mashariki
kuwa na barabara zenye lami kwa kilomita nyingi. Lakini pamoja na mafanikio
hayo, nchi imekuwa ikikumbana na changamoto mbalimbali katika kila hatua ya
kujaribu kuboresha huduma na mahitaji ya kijamii.
Miongoni
mwa changamoto hizo ni usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na ubora wa
huduma zinazotolewa. Viwango vya ubora kwa huduma zinazotolewa, vimekuwa
vikipungua kadri siku zinavyokwenda na sababu kubwa ni udhaifu wa usimamizi
kutoka kwa mamlaka husika.
Udhaifu
huu umesababisha wananchi ambao kimsingi ndiyo walipa kodi za serikali
kulalamika kila siku. Ikumbukwe kuwa ukusanyaji mzuri wa kodi na kuweka
matumizi wazi husaidia kuboresha huduma mbalimbali ndani ya jamii.
Ili
kuepukana na utawala mbovu usiojali wala kuheshimu misingi ya utawala bora,
kuna haja ya wananchi kufanya kazi pamoja. Hapa ndipo tunapouona mpango wa
Chukua Hatua kama mkombozi kupita uraghbishi, yaani kuwahuisha na kuwahamasisha
watu walionyimwa haki kujiona kama watendaji wakuu na siyo kama watu wa chini
mbele ya matabaka mengine.
Ni
sahihi, kuona wananchi wakisimama imara, kujithamini na kujenga uelewa wa
misingi ya uchambuzi wa hali ya maisha yao. Lakini pia, kuwawezesha watu kuwa na
utamaduni wa kuthubutu kujaribu mambo mbalimbali ya maendeleo. Watu hao tunawaita
waraghbishi.
Waraghbishi hawa wameanza uraghbishi tangu mwaka 2010
pale mpango wa Chukua Hatua ulipoanza katika wilaya za Bukombe, Kahama,
Shinyanga Vijijini, Maswa, Kishapu na Bariadi.
Ziliongezeka wilaya mbili, Itilima na Mbogwe baada ya
baadhi ya wilaya za Mkoa wa Shinyanga kuhamishiwa mikoa mipya ya Geita na
Simiyu na wilaya ya Ngorongoro kwa mkoa wa Arusha.
Uraghbishi
ulianza kwa kikundi cha watu wasiozidi 15 kupitia Mtandao wa Vikundi vya
Wakulima Tanzania (MVIWATA) katika mkutano wa kimkakati uliofanyika katika Chuo
cha Ushirika tawi la Shinyanga, mwezi Septemba mwaka 2010. Miongoni mwao ni
aliyekuwa Mwenyekiti wa mtandao kwa Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Titus
Ndugulile kutoka kijiji cha Mwamala.
“Ni vigumu
kuamini kama mpango huu umekuwa mkubwa kiasi hiki. Tulianza watu 12 tu miaka
mitano iliyopita, lakini leo tupo waraghbishi zaidi ya 400. Kwa hakika haya ni
mafuriko ya waraghbishi, kwani sasa kila sehemu wanapatikana,” alisema
Ndugulile.
Viongozi wa mitandao ya wilaya za Bukombe na Mbogwe mkoani Geita wakiwa katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika kata ya Masumbwe hivi karibuni |
Baada ya kikao
hicho, yalifuata mafunzo maalumu ya uraghbishi kwa siku tatu yakiendeshwa kila
wilaya. Mafunzo hayo yalilenga kufundisha namna ya kutafuta na kupata taarifa
na kutambua changamoto zinazoikabili jamii na njia za kuzitatua.
“Nilikwenda ofisi zetu za halmashauri kuulizia vyanzo
vya mapato vya wilaya na kuelezwa kuwa Mgodi wa Mwadui hauchangii chochote
pamoja na kuwa upo katika eneo hilo. Taarifa hii niliwashirikisha na wenzangu
pia.”
Mraghabishi toka kijiji cha Negezi wilayani Kishapu Fredina Said amekuwa chachu ya maendeleo katika kijiji chake |
Hayo ni maneno ya mraghbishi Fredina Said kutoka kijiji
cha Negezi, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga. Pamoja na kwamba hakuweza kulifikisha mbali suala
hilo, angalau aliweza kufahamu kilichokuwa kikiendelea.
Pamoja na mambo hayo, walifundishwa pia namna ya
kujiamini kupitia mafunzo ya uraghbishi waliyokuwa wakiyapata kwa mara ya
kwanza. Mafunzo haya yalitolewa kwa nadharia na vitendo ambapo
waraghbishi baada ya kupatiwa mafunzo ya darasani walipewa kazi ya kutembelea
ofisi za halmashauri za wilaya zao.
Lengo ni moja tu, kuwajengea uwezo wa kuongea na
viongozi wa kitaifa kama mkuu wa wilaya au mkurugenzi baada ya awali kuonyesha
hofu na kutojiamini.
“Ilikuwa mara ya kwanza kuonana na mkuu wa wilaya na
kumuulizia masuala ya pembejeo za kilimo. Nilikuwa na hofu, hata hivyo kinyume
na matarajio yangu, maswali yote aliyajibu ingawa siyo kwa kiwango nilichotarajia,”
alisema mraghbishi Fedson Yaida wa Kijiji cha Shenda, wilaya Mbogwe, mkoani
Geita.
Matokeo ya kutembelea ofisi hizo yalionekana pale
walipopatiwa majibu ya maswali yao.
Kazi hii ilikuwa na umuhimu mkubwa katika kuwandaa
waraghbishi na majukumu makubwa ya uraghbishi. Waraghbishi hawa walikuwa
wakiwakilisha wananchi wa vijiji vyao, hivyo moja ya jukumu lao ilikuwa ni
kuwashirikisha walichojifunza.
Jukumu hilo walilifanya vizuri na waliweza kutambuliwa
kwa urahisi na viongozi wa vijiji pamoja na wananchi wenzao.
Na kwa sababu walipatiwa mafunzo kupitia mradi wa
Chukua Hatua, walijikuta wakiitwa kwa jina hilo hilo la Chukua Hatua. Mfano
mzuri ni waraghbishi waliopo katika kijiji cha Mwime, wilayani Kahama mkoani
Shinyanga.
Hali hii ilisababisha wananchi wengi katika vijiji ambavyo
mradi wa Chukua Hatua unaendeshwa kujitambulisha kama waraghbishi na kutaka na
wao wapatiwe mafunzo. Na hapo ndipo lilipokuja wazo la kuwawezesha waraghbishi
wa zamani na wapya kufanya kazi kwa pamoja.
Mraghbishi kutoka Kijiji cha Ololosokwani, Kootu Tome,akigawa majarida yenye riwaya za za chukua hatua kwa wanakijiji wenzake |
Akielezea jinsi alivyowafundisha waraghbishi jinsi ya
kufanya uraghbishi katika kijiji chake na vile vya jirani, mraghbishi kutoka
Kijiji cha Ololosokwani, Kootu Tome, alisema:
“Nimefundisha waraghbishi wa kijiji cha jirani.
Niliwaeleza maana ya uraghbishi, kwamba hawatakiwi kujionyesha wazi kwa kila
jambo, badala yake wanawashawishi watu kuchukua hatua katika kile anachokuwa
amewafafanulia,”
Mraghbishi
mwingine ni Julius Katende kutoka Kijiji cha Ngarwa, wilayani Ngorongongo
aliwafundisha waraghbishi wapya tofauti ya uraghbishi na uhamasishaji.
Mraghbishi si mwamasishaji, bali ni mtu anayeibua hoja katika jamii na
kuzitafutia majibu kwa kushirikiana na wenzake.
Jumla
ya waraghbishi wapya 762 wamefundishwa na waraghbishi 322 wa zamani, ikiwa ni
ongezeko mara mbili katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Julai hadi
Septemba na kufanya idadi yao kuwa 1,084. Kati yao, wanawake ni zaidi ya 400.
Hili ni ongozeko kubwa ambalo ni wazi linatokana na juhudi za pamoja.
“Tuliwafundisha
kutoka katika maeneo mbalimbali ambayo wamekuwa na kawaida ya kukusanyika,” haya
ni maneno ya mkurugenzi wa Tamasha, Richard Mabala, wakati akifafanua namna
wanavyoendesha mafunzo hayo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Waraghbishi
kwa upande mmoja wanawakilisha wananchi wa maeneo yao na wamekuwa mstari wa
mbele kusimamia rasilimali zao na kuhakikisha huduma bora za jamii
zinapatikana. Lakini ili kufanikisha, malengo ya mpango wa Chukua Hatua,
viongozi wa vijiji, hasa wenyeviti, watendaji wa kata na vijiji wanafundishwa uraghbishi
pia kulingana na nafasi zao.
Mkurungezi wa CABUIPA David Rwegoshora akifafanua jambo katika mkutano uliokutanisha waragahbishi toka mikoa ya Shinyanga ,simiyu na Arusha |
Jukumu
la kuwafundisha viongozi hawa kwa upande wa mikoa ya kanda ya ziwa wamepewa
CABUIPA, shirika mdau la mpango wa Chukua Hatua lilipo Kahama. Akifafanua
wanachofanya, mkurugenzi wa shirika hilo, David Rwegoshora alisema:
“Katika
kipindi cha miezi mitatu tumefundisha wenyeviti 167 na watendaji 33 ngazi ya
kata. Kati yao, wanawake walikuwa sita.”
Waraghbishi toka kijiji cha Pandagichiza wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya tanki la maji, ambalo baadhi yao ndio wasimamizi wake kutokana uaminifu wao |
Kwa
upande wa Ngorongoro, wenyeviti 14, watendaji 14 wa vijiji na 6 wa kata
walipatiwa mafunzo hayo. Kundi lingine ni Sungusungu, ambapo hadi sasa idadi
yao ni 15 nao walipewa mafunzo hayo ya uraghbishi. Wote hawa ni waraghbishi kwa
nafasi zao. Katika awamu iliyopita ilijumuisha na viongozi wa dini wakiwamo
masheikh, maimamu, wachungaji na makatekista.
Katika
kuhakikisha waraghbishi wanawafikia watu wengi zaidi na kuwafundisha
uraghbishi, mitandao ya waraghbishi imeanzishwa katika wilaya za Mbogwe,
Kahama, Maswa, Kishapu, Bariadi, Shinyanga Vijijini, Itilima na Bukombe.
Mitandao hii ilianza rasmi mwaka 2014 na kuwaleta pamoja waraghbishi wa mikoa
ya Geita, Simiyu na Shinyanga.
Hadi sasa, kuna wenyeviti pamoja na wasaidizi wao,
ambao idadi yao imefikia 32, wanawake 16, sawa na asilimia 50. Wingi huu wa
waraghbishi hauangalii itikadi za vyama, badala yake unaangalia kilicho bora kwa
wanajamii kwa ujumla.
CHANZO; MWANAHARKATI MZALENDO
Post a Comment