Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Rais na Ofisa mtendaji Mkuu wa kampuni ya Sumitomo
Corporation ya Japan, Bw. Kunihuru Nakamura katika Mkutano wa TICAD 6
uliofanyika Nairobi Kenya, Agosti 28, 2016. (Pivha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais na Ofisa
mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sumimoto Corporation ya Japan katika mkutano
wa TICAD 6 uliofanyika jijini Nairobi Agosti 28,2016. (Picha na ofisi
ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwa katika picha ya pamoja na Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni
ya Sumimoto ya Japan, Bw. Kanihuru Nakamura (kushoto kwake) baada ya
mazungumzo yao jijini Nairobi Agosti 28, 2016. Kushoto ni Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa James Mdoe na Kulia ni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dkt.Adelhelm
Meru. Wanne kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mathias
Chikawe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akisalimiana na Balozi wa Umoja
wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Wakimbizi, Fillipo Grand kabla
ya mazungumzo yao jijini Nairobi, Agosti 28, 2016. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikabidhiwa kitabu chenye picha ramani na taarifa za jiji la Yokohama
nchini Japan na Meya wa jiji hilo, Bi. Fumiko Hayashi baada ya
mazungumzo yao jijini Nairobi Agosti 28, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa TANTRADE, Bw. Edwin
Rutageruka (kushoto) wakati alipotembelea banda la Tanzania katika
maonyesho yaliyokwenda sambamba na mkutano wa TICAD 6 jijini Nairobi
Agosti 28, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akimsikiliza , Bw. Lameck Borega (kushoto) ambaye ni Meneja wa
Uwekezaji kutoka EPZA, Mabibo jijini Dar es salaam wakati alipotembelea
banda la Tanzania katika maonyesho yaliyokwenda sambamba na mkutano wa
TICAD 6 jijini Nairobi Agosti 28, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitazama pipili iliyosindikwa na kupewa jina la AKABANGA wakati
alipotembelea banda la Rwanda katika maonyesho yaliyokwenda sambamba na
mkutano wa TICAD 6 jijini Nairobi Agosti 28, 2016. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na washiriki wa maonyesho kutoka Senegal wakati
alipotembelea bada lao kwenye maonyesho yaliyokwenda sambamba na
mkutano wa TICAD 6 jijini Nairobi Agosti 28, 2016. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitazama nguo za batik wakati alipotembelea banda la Tanzania kwenye
maonyesho yaliyokwenda sambamba na mkutano wa TICAD 6 jijini Nairobi
Agosti 28, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewakaribisha wawekezaji kutoka Japan na kusema kwamba kufanyika kwa
Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Bara la Afrika
(TICAD VI) jijini Nairobi kumetoa fursa kwa Tanzania na nchi nyingine
kukutana na wafanyabiashara wakubwa wenye nia ya kuwekeza barani humo.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumapili,
Agosti 28, 2016) alipokutana faragha kwa nyakati tofauti na viongozi wa
makampuni makubwa ya Japan ambao walikuwa wakihudhuria mkutano huo
uliofanyika katika kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Jomo Kenyatta
(JICC) jijini Nairobi, Kenya.
Mkutano wa sita wa TICAD ambao
umemalizika jana, ulilenga kuiwezesha Afrika katika sekta ya uchumi na
uwekezaji. Ili kufikia lengo hilo, mkutano huo umewashirikisha wadau wa
sekta binafsi zikiwemo kampuni binafsi zaidi ya 300 kutoka Japan.
Katika mazungumzo yake na Waziri
Mkuu, Rais wa kampuni ya Sumitomo, Bw. Kuniharu Nakahura, alisema
kampuni hiyo imeanza utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi II wa kuzalisha
umeme wa MW240 kutoka gesi asilia (Gas Fired Combined Cycle Gas Power Plant). Mradi huo ulioanza kutekelezwa Machi 2016, unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.
Bw. Nakahura ambaye pia ni Afisa
Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, alisema kampuni yao inajishughulisha
zaidi na utengenezaji wa bidhaa za vyuma, kemikali, ujenzi wa
miundominu, na usafirishaji.
Naye Makamu wa Rais wa kampuni ya
Toyota Tshuso, Bw. Yasuhiko Yokoi alikutana na Waziri Mkuu na kumweleza
jinsi kampuni hiyo kubwa duniani inavyoweza kushiriki na kuchangia
maendeleo nchini Tanzania.
Alisema kampuni yao
inajishugulisha zaidi na masuala ya miundombinu ikiwemo kuzalisha
mitambo ya umeme na mitambo ya bandari. Pia inazalisha bidhaa za kilimo
(matrekta, mashine za viwanda vya mbolea na nguo, ujenzi wa maghala ya
nafaka), mitambo ya nguvu za umeme wa joto-ardhi na uzalishaji wa magari
ya aina mbalimbali.
“Kwa mfano hapa Kenya, tumeweza
kutengeneza mitambo midogo ya kisasa ambayo inazalisha mbolea tofauti
kulingana na hali halisi ya udongo wa mahali husika. Huwezi kuzalisha
mbolea ya aina moja na kuamua kuisambaza kwa nchini nzima. Tunapima
udongo wa sehemu moja na kuzalisha mbolea inayofaa kwa udongo ule,”
alisema.
Naye Rais wa kampuni ya Marubeni,
Bw. Fumiya Kokubu alimweleza Waziri Mkuu kwamba maeneo ambayo wangependa
kuwekeza ni kwenye viwanda vya nguo, mbolea, saruji, uzalishaji wa
sukari, umeme wa gesi na hasa miradi ya LNG.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu
aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali iko tayari kushirikiana nao
na akawashauri watume timu za maafisa wao ili wakutanishwe na wadau wa
sekta husika.
Alisisitiza kuwa Tanzania hivi
sasa imedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa viwanda na kwa sababu hiyo
inahitaji kuwa na nishati ya kutosha ili iweze kumudu kuendeleza sekta
hiyo. “Serikali ya awamu ya tano imeamua kujenga uchumi wa viwanda,
tunahitaji kujenga viwanda vya kutosha ili tuweze kusindika mazao ya
wakulima ambao wanafikia asilimia 80 ya Watanzania wote. Tunahitaji
masoko ya uhakika kwajili ya mazao wanayozalisha,” alisema.
Akiwa kwenye mkutano huo, Waziri
Mkuu pia alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Mataifa
anayeshughulikia masuala ya wakimbizi, Bw. Filippo Grandi; Meya wa Jiji
la Yokohama, Bibi Fumiko Hayashi; na Makamu wa Rais wa Kwanza wa Sudan,
Jenerali Bakri Hassan Saleh.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
alitembelea Maonesho ya Biashara ya Afrika na Japan (Africa-Japan Expo
2016) ambapo Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TANTRADE) na wadau
wengine kama Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza
Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya
Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) walishiriki.
Akiwa huko alitembelea pia mabanda
ya Uganda, Rwanda, Sénégal, Kenya, Japan na UN Habitat. Pia alitembelea
banda la wajasiriamali wa nguo kutoka Tanzania ambao walishiriki
maonyesho hayo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kituo cha Mikutano ya
Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JICC) jijini Nairobi, Kenya.
Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam jana usiku.
Post a Comment