Na Jumia Travel Tanzania
HAKUNA jambo linalokera kama kugundua kuwa umesahau kitu fulani ambacho kilikuwa kina umuhimu mkubwa sana kwenye safari yako uliyokwishaianza.
Hali kama hii huwa inawatokea watu wengi hivyo kupelekea kuchelewa au wakati mwingine kuachwa kabisa na usafiri.
Kuepukana na usumbufu huu hasa ukizingatia asilimia kubwa ya watu wako kwenye pilikapilika za kusafiri kipindi hiki cha sikukuu na shamrashamra za mwaka mpya, Jumia Travel (www.travel.jumia.com) ingependa kukutahadharisha kuzingatia yafuatayo ili safari yako iwe ya raha mustarehe.
Tafiti kuhusu mahali unapokwenda
Ni muhimu kufahamu mahali unapokwenda hasa umbali wake, itakugharimu kiasi gani kufika, hali ya hewa, gharama za maisha pamoja na mila na utamaduni za watu wanaoishi huko. Kama unasafiri mkoa ambao haujawahi kufika hapo awali ni vizuri ukafanya tafiti au ukaulizia kutoka kwa marafiki, ndugu na jamaa ili usiende kupata tabu ukifika.
Tambua usafiri utakaokufikisha huko
Zipo njia nyingi za usafiri za kuweza kukufikisha mahali unapotaka inategemea chaguo, uharaka au uwezo ulionao. Kama unataka kuwahi mahali unapokwenda kutokana na shuguli nyingi au kuepuka uchovu basi usafiri wa anga (ndege) utakuwa ni sahihi kwako. Na kama hautojali kuwahi au uchovu njia ya barabarani kwa kutumia basi itakufaa kwani utaweza kuwa na muda wa kutosha kujionea vitu vingi njiani vitakavyopelekea kunogesha safari yako.
Kata tiketi mapema siku moja kabla ya safari
Usipendelee kukata tiketi siku ya safari kwani unaweza kukuta usafiri haupatikani, nafasi zimejaa, bei imebadilika au kupata basi ambalo halikuridhisha na hadhi yake. Kata tiketi siku moja kabla ya safari kwani itakuondolea hofu ya kutokuwa na uhakika wa kusafiri na kukupa muda wa kupanga mambo mengine vizuri zaidi.
Panga vitu unavyovihitaji kwa ajili ya safari mapema
Kutojipanga mapema na safari mara nyingi hupelekea mtu kusafiri huku akiwa ameacha vitu muhimu huko mbele aelekeapo. Na kamwe usijidanganye kwamba utaweza kumudu kukumbuka na kupanga vitu vyako vyote unavyovihitaji siku ya safari kwani unaweza ukachelewa kuamka na ukahamaki mwishowe ukajikuta unasahau kubeba vitu vya msingi. Hivyo tunakushauri weka kila kitu unachokiona ni muhimu kwa safari yako ndani ya begi siku moja kabla ya safari bila ya kusahau kuiweka tiketi yako sehemu ambapo unaiona kwa urahisi.
Fahamu mahali utakapolala pindi utakapowasili
Siku hizi huhitaji kusumbukaili kufahamu sehemu ya malazi kwa sababu taarifa zote zinapatikana kwa njia ya mtandao. Kwa mfano, ukitembelea mtandao wa Jumia Travel (www.travel.jumia.com) utaweza kuperuzi orodha ya hoteli na sehemu mbalimbali za malazi nchini, utafahamu mahali ziliko, hadhi zake, gharama, upatikanaji na namna ya kulipia.
Amka mapema na wahi kituoni siku ya kusafiri
Kama una mazoea ya kuchelewa kuamka asubuhi ni vema ukaweka kengele ikuamshe asubuhi kupitia simu au kifaa ulichonacho au kumtaafiru ndugu au rafiki akuamshe mapema. Kuamka mapema kunakuwezesha kujiandaa vya kutosha kwa safari hata kukupa kuda wa kukumbuka vitu ambavyo pengine ulivisahau pamoja na kuwahi kituoni tayari kwa kusafiri.
Kuwa makini na vyakula unavyokula njiani
Huna budi kuzingatia aina ya vyakula utakavyokuwa unakula njiani kwani vinaweza kukudhuru kiafya. Vyakula vinavyopikwa na kuuzwa njiani huna uhakika vinaandaliwa vipi na kupikwa katika mazingira gani hivyo umakini mkubwa unahitajika. Hata hivyo, kutokana na maboresho ya miundombinu siku hizi safari nyingi hazichukui muda mrefu kwa hiyo unaweza ukala vyakula vikavu kama vile keki au mikate pamoja na vinywaji kama maji, soda au juisi mpaka utakapofika ndipo ule chakula cha kutosha.
Jihadhari usiachwe na basi njiani
Kuna matukio kadhaa ambapo abiria huachwa na usafiri hususani kwenye vituo vifupi vinavyowekwa njiani kuwapa fursa abiria kujisaidia au kununua chakula. Kama unajijua ni mzito kula kituoni ni vema ukanunua, ukabeba chakula na kwenda kulia ndani ya basi vilevile kwa kujisaidia nakushauri jisaidie mahali ambapo utaliona basi au abiria unaosafiri nao ili isiwe rahisi kuachwa.
Tunatumaini kwamba mbinu hizi chache zitakusaidia pakubwa katika safari yako unayoitarajia msimu huu wa sikukuu.
Post a Comment