Serikali
kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa ufafanuzi wa uamuzi wake wa
kuzuia biashara ya usafirishaji wa wanyamahai nje ya nchi kwa kipindi
cha miaka mitatu mfululizo na kusema kuwa uamuzi huo ulitolewa kwa lengo
la kupanga vizuri biashara hiyo kwa faida ya serikali na
wafanyabiashara wenyewe.
Ufafanuzi
huo umetolewa jana na Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Jumanne Maghembe
katika kikao alichokiitisha wizarani hapo na wafanyabiashara wa
wanyamahai wa makundi ya wadudu, vyura, mijusi, ndege, nyani na tumbili
ambao walitaka kupata ufafanuzi wa hatima ya biashara yao kutoka
serikalini.
Katika
risala iliyosomwa na kiongozi wa wafanyabiashara hao, Adam Rashid
Warioba kwa Waziri Maghembe, aliiomba Serikali kutoa ufafanuzi wa hatma
ya biashara yao iliyofungiwa ambayo imekuwa tegemeo pekee katika
kuendesha maisha yao huku wakitaka kujua hatma ya wanyamahai
waliohifadhiwa na gharama zao walizolipia Serikalini.
Akitoa
ufafanuzi wa uamuzi wa Serikali kufungia biashara hiyo kwa
wafanyabiashara hao, Prof. Maghembe amesema wanyamahai wengi kutoka
nchini Tanzania wamekuwa wakisafirishwa nje ya nchi bila ya kufuata
utaratibu maalum ikiwemo vibali vya kukamata na kuwasafirisha wanyama
hao jambo ambalo limekuwa likiikosesha serikali mapato mengi.
“Wapo
kati yenu ambao walikuwa wanasafirisha wanyamahai kinyume cha sheria,
bila vibali vyovyote, na wanyama wa Tanzania walikuwa wakimatwa kwenye
bandari na viwanja vya ndege, ambao wanasafirishwa kinyume cha sheria,
wengi tu, na ndio maana Serikali ikasema hii biashara tusimamae kwanza
tuwekwe utaratibu ambao kila mtu ataufuata, na ambao hautaweza kututia
aibu huko nje” alisema.
Alisema
sababu nyingine iliyopelekea serikali kufunga biashara hiyo kwa muda ni
bei ndogo inayouzwa wanyama hao nje ya nchi ambayo haiwanufaishi
wafanyabiashara na Serikali ukilinganisha na thamani yake kwa kile
wanachoenda kufanyiwa, alitolea mfano tumbili ambao hufanyiwa utafiti wa
madawa mbali mbali na baadae kuuzwa mabilioni ya fedha huku tumbili
huyo akiuzwa kwa dola 25 tu.
“Nimefurahi
yule bwana aliyesema tumbili mmoja ni dola 25, lakini akasema hao ndio
wanafanyamedical research (utafiti wa madawa) yote duniani, sasa sisi
tunapata dola 25 na wenzetu wanafanya research (utafiti) wanatuuzia
madawa yote billions of dollars (mabilioni ya dola za kimarekani),
tuweke utaratibu na ninyi mtakapokuwa mnafanya hii biashara mpate sio
lazima serikali ndio lazma ipate, mpate kilicho sawa na thamani ya
wanyama mnaowauza”, alisema Prof. Maghembe.
Aliwahakikishia
wafanyabiashara hao kuwa Serikali ya awamu ya tano ni sikivu hivyo
kuahidi kushuulikia changamoto walizoziwasilisha hadi kufikia Januari
10, mwakani (2017), aliwaeleza kuwa hatma ya wanyamahai ambao
wamewahifadhi pamoja gharama za vibali walizowalipia serikalini
zitashuulikiwa.
“Ambacho
ninaweza kuwaambia hapa leo, kwamba tumepata hii taarifa, tunayo ile
idadi ambayo imepitiwa na wataalamu huko kwenye mazizi, tunazo zile
permit (vibali) za serikali ambazo mmepewa na leseni, vyote vile
mlivyonavyo na sisi tunavyo, tutavipitia vyooote kabisa, alafu tutaona
ni namna gani tutawainua kwa kuwafuta jasho”, alisema.
Aliongeza
kuwa “Tutaangalia kila mfanyabiashara ameilipa nini serikali, kwa
wanyama hawa ambao wapo, ambao katazo lilipofanywa walikuwa nao kwenye
mazizi yao na wanyama hao tunawafanyia tathmini tukishakamilisha
tutaamua sasa wanyama hao wanapelekwa wapi, na maeneo yenyewe ni
machache tu, ama kwenye mazoo, ili waweze kutunzwa na kuendelezwa kwa
vile ni vigumu kuwarudisha tena maporini.
“Na
kutokana na vibali na risiti mbalimbali ambazo wameilipa serikali katika
kuwapata hao wanyama basi tutaviangalia na kuangalia utaratibu wa
kuwarudishia wale wafanyabiashara hela zao”.
Akizungumzia
lalamiko la wafanyabiashara hao kuwa wao wamezuiliwa kufanya biashara
hiyo huku mfanyabiashara mmoja kutoka nje akiruhusiwa kufanya biashara
hiyo kwa tangazo la serikali, Prof. Maghembe anasema “Na hilo tangazo
mnalosema lina mtu amebebwa hamna ruhusa ya mtu kubebwa hapa, na mtu
atayempa huyo mtu kibali mnafahamu kitakachotokea, hakuna ruhusu, ndivyo
serikali ilivyosema”.
Mei 26,
mwaka huu, akifanya majumuisho ya hotuba ya Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2016/17, Waziri wa Maliasili na
Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, alitangaza kuwa ni marufuku kusafirisha
wanyamahai wote nje ya nchi kwa miaka mitatu mfululizo.
“Kuanzia
sasa (saa moja na dakika tano usiku) kwa miaka mitatu serikali imepiga
marufuku usafirishaji wa wanyamahai wote kwenda nje ya nchi, hata chawa
wa Tanzania hawataruhusiwa kusafirishwa nje, Na katika kipindi hiki cha
miaka mitatu, idara ya wanyamapori itafanya kazi ya kuishauri serikali
namna gani biashara hiyo itakavyoendeshwa”, alisema Prof. Maghembe.
Imetolewa na;
Hamza Temba
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Maliasili na Utalii
Post a Comment