Kamati
za Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) katika Shule za Msingi za Serikali
nchini zimefanikiwa kudhibiti utoro, nidhamu na kutofanya vizuri kwa
baadhi ya Wanafunzi katika shule hizo kwenye mitihani yao ya kumaliza
Elimu ya Msingi. Lilian Lundo wa Idara ya Habari (MAELEZO) anaelezea.
Mwaka
2015 Serikali kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania
(Education Quality Improvement Programme –Tanzania (EQUIP-T), ilianzisha
Kamati za Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) katika shule za msingi nchini
kwa lengo la kujenga uhusiano mzuri kati ya Walimu na Wazazi ikiwa ni
njia mojawapo ya kuinua ubora wa elimu.
Aidha,
Kamati hizo zilipewa jukumu la kufuatilia maendeleo ya Kitaaluma kwa
Wanafunzi, kubuni miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya shule na
kubuni klabu mbalimbali ambazo zitawashirikisha Wananfuzi katika
kujadili masuala ya kijamii na hivyo kuwavutia Wanafunzi kupenda masomo.
Mpango
huo ambao awamu ya kwanza ulianza katika mikoa ya Dodoma, Kigoma,
Lindi, Mara, Simiyu, Shinyanga na Tabora, umeleta mafanikio makubwa
kimaendeleo ya kitaaluma darasani, kuongezeka kwa nidhamu na kudhibiti
utoro jambo ambalo pia limeongeza ufaulu katika mitihani yao ya Elimu ya
Msingi.
Kwa
mujibu wa wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Uhelela iliyoko Wilaya ya
Bahi mkoani Dodoma Bw. Dankan Kamwela, mpango huo umepata mafanikio
makubwa katika shule yake ambapo imefanikiwa kupunguza utoro kutoka
Wanafunzi 127 sawa na asilimia 30 kwa siku mwaka 2015 hadi Wanafunzi 12
sawa na silimia 8 kwa siku mwaka 2016.
Ameelezea
kwamba, kwa kuitumia Kamati ya Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) wamekuwa
wakifanya vikao mara kwa mara kwa kuwashirikisha Wazazi na Wanafunzi
kujadili maendeleo ya Shule ikiwa ni pamoja na wajibu wa Walimu, Wazazi,
na Wanafunzi kwa ujumla.
Amesema,
kufuatia vikao hivyo ilibainika kuwa iko haja ya kuweka mikakati
itakayosaidia kurekebisha kasoro zote zilizoonekana kuchangia kushuka
kwa maendeleo ya kitaaluma, utoro na nidhamu ambavyo kwa pamoja
vinasabisha kutofanya vizuri kwa Wananfunzi katika mitihani yao kwenye
shule zilizo katika Kata hiyo.
Kwa
upande wake, Afisa Elimu Mkoa wa Mara Bw. Hamis Lissu amesema ufaulu wa
darasa la saba mkoani humo umekuwa ukipanda mwaka hadi mwaka kuanzia
mwaka 2014. Ameeleza kuwa mwaka huo mkoa wa Mara ulikuwa katika nafasi
ya 25 kati ya mikoa 25. Mwaka 2015 mkoa wa Mara ulishika nafasi ya 17
kati ya 25 na mwaka 2016 umeshika nafasi ya 13 kati ya mikoa 26.
Mratibu
Elimu Kata wa Chamwino, Chitema Simango amesema kuwa Kamati hiyo
imewezesha kwa kiasi kubwa ushiriki wa Wazazi katika maendeleo ya shule
ambapo kabla ya kuanzishwa Umoja huo Walimu walikuwa wakiachiwa
ufuatiliaji wa maendeleo ya Wanafunzi pamoja na shule lakini kwa sasa
Wazazi na Walimu wanashirikiana kwa katika kufuatilia maendeleo ya
Wanafunzi na shule kwa ujumla.
Vile
vile amesema kuwa UWW umeleta uwazi katika mapato na matumizi ya Shule
ambayo yanabandikwa katika mbao za matangazo za shule husika na Wazazi
wanapewa nafasi ya kuhoji juu ya mapato na matumizi hayo.
Aidha
ametoa ushauri kwa Maafisa Elimu, Waratibu Elimu Kata na Walimu Wakuu
katika mikoa ambayo bado haijaanzisha Kamati za UWW kuanzisha Kamati
hizo katika shule zao ili kuleta mabadiliko ya uendeshaji wa shule za
msingi za Serikali kwa kuishirikisha jamii. Kwani kupitia UWW Walimu na
Wazazi wanajadiliana kwa pamoja na kukubaliana namna ya kuboresha
taaluma ya Wanafunzi katika shule husika na hata katika kusimamia miradi
ya shule.
Pia
amesema kuwa Wazazi wanaposhirikiana na walimu inapelekea Wanafunzi kuwa
na nidhamu ya hali ya juu kutokana na mwanafunzi asiye na nidhamu au
mtoro anakosa pakukimbilia kwani mwalimu na mzazi wamekuwa kitu kimoja.
Mpango
wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (Education Quality Improvement
Programme -Tanzania) EQUIP-T ni mpango unaosimamiwa na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kudhaminiwa na Serikali ya Uingereza.
Mpango huu ni wa miaka minne ambao ulianza mwaka 2014 katika mikoa ya
Dodoma, Tabora, Simiyu, Shinyanga, Kigoma, Mara na Lindi.
Mpango
huo umejikita katika kuinu ubora wa Elimu Shule za Msingi katika nyanja
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu wa madarasa ya
awali mpaka la tatu katika kuwajengea uwezo katika ufundishaji, utoaji
wa vifaa vya kufundishia, uanzishwaji wa kamati za walimu na wazazi
pamoja na mafunzo ya uongozi kwa walimu wakuu, kamati za shule pamoja na
umoja wa walimu na wazazi.
Post a Comment