Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini agizo rasmi la rais kupiga marufuku kutolewa kwa pesa za serikali ya Marekani kufadhili mashirika ya nchi za nje ambayo yanatekeleza au kutoa habari kuhusu utoaji mimba.
Afisa wake wa mawasiliano Sean Spicer amesema hatua hiyo ya rais inaonesha kwamba "anataka kuwatetea Wamarekani wote, wakiwemo wale ambao hawajazaliwa."
Agizo hilo ambalo kirasmi linafahamika kama "the Mexico City Policy" (Sera ya Jiji la Mexico) huenda likayakera makundi ya kutetea uhuru wa wanawake kuamua kuhusu uzazi, ambayo tayari yametiwa wasiwasi na msimamo wake wa kupinga utoaji mimba.
Bw Trump anaunga mkono utoaji mimba upigwe marufuku Marekani.
Lakini hii si mara ya kwanza kwa marufuku dhidi ya ufadhili wa mashirika ya utoaji mimba nje ya Marekani kutolewa.
Rais wa Republican Ronald Reagan mara ya kwanza alianzisha Sera ya Jiji la Mexico mwaka 1984 na kuwa wa kwanza kupiga marufuku ufadhili huo.
Lakini chama cha Democratic kilibatilisha marufuku hiyo chini ya utawala wa Bill Clinton.
Sera hiyo inayataka mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanapokea ufadhili wa serikali ya Marekani kukubali "kutotekeleza na kutoendeleza au kutohamasisha watu watumie utoaji mimba kama njia ya uzazi wa mpango katika nchi nyingine".
Kwa miongo mingi, imekuwa kwamba pesa za Marekani haziwezi kutumiwa katika utoaji mimba katika mataifa ya nje.
Lakini Sera ya Jiji la Mexico inaenda hatua zaidi.
Haki miliki ya picha Getty Images
Mwaka 2009, Barack Obama alisitisha utekelezaji wa sera hiyo, ambayo ilikuwa imrejeshwa chini ya utawala wa Rais George Bush.
Makundi ya kutetea uhuru wa wanawake kuamua kuhusu uzazi wamepinga hatua hiyo ya Bw Trump.
"Ni jambo la kusikitisha sana kwamba moja ya hatua za kwanza za Trump inaunganisha mambo mawili kwa pamoja: kunyamazisha wote wanaotofautiana naye na kuwakandamiza wanawake," taarifa kutoka kwa kundi la Naral Pro-Choice America imesema
"Siku mbili baada ya maandamano ya kihistoria ya wanawake ya kumpinga Trump kufanyika na siku moja baada ya maadhimisho ya uamuzi wa kihistoria wa mahakama kesi ya Roe v. Wade, Donald Trump anapatia kipaumbele hatua ya kurejesha ... sera ambayo inawanyamazisha wahudumu wa afya na kuweka hatarini wagonjwa."
Wakati wa kampeni, Bw Donald Trump, ambaye awali alitetea uhuru wa wanawake kuamua kuhusu uzazi, aliambia MSNBC kwamba "lazima kuwe na aina fulani ya adhabu kwa mwanamke" iwapo utoaji mimba utakuwa marufuku.
Baadaye, aliondoa tamko hilo baada ya kushutumiwa vikali na makundi ya kutetea haki za wanawake.
Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Agizo hilo limetolewa siku mbili baada ya wanawake kuandamana Washington na miji mingine kumpinga Trump
Maafisa wa kampeni wa Bw Trump walisema waliamini uamuzi kuhusu uhalali wa utoaji mimba unafaa kuachiwa majimbo yenyewe, na kwamba adhabu inafaa kutolewa kwa wanaotoa huduma za utoaji mimba.
Alisema anaunga mkono marufuku ya utoaji mimba ila tu wakati mimba imetokana na "ubakaji, kujamiiana kwa maharimu au wakati maisha ya mama yamo hatarini".
Bw Trump pia ameahidi kujaza nafasi ya jaji iliyo wazi Mahakama ya Juu na jaji ambaye ni mhafidhina kuhusu masuala ya kijamii.
Hayo yakijiri, Bunge la Congress limeashiria nia yake ya kuondoa ufadhili wa serikali kwa kundi la Planned Parenthood, kundi linalotoa huduma za afya ya uzazi Marekani na nje ya taifa hilo.BBC SWAHILI


Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top