Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Joseph
Magufuli, kesho tarehe 25 /01/2017 anatarajiwa kuzindua Awamu ya Kwanza
ya Miundombinu na Utoaji wa Huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka (Bus Rapid
Transit – BRT) katika Kituo Kikuu cha Mabasi kilichopo Kariakoo eneo la
Gerezani.
Uzunduzi huo utahudhuriwa na Rais
wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika, Bw. Makhtar Diop na Mkurugenzi
Mkazi wa Benki ya Dunia wa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia
Bi. Bella Bird.
Awamu ya Kwanza ya mradi wa
ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) yenye urefu wa
kilometa 20.9 unaojumuisha barabara ya Kimara – Kivukoni, Magomeni –
Morocco na Fire – Kariakoo ulikamilika Desemba 2015.
Aidha, utoaji wa huduma ya Mabasi
Yaendayo Haraka ulianza tarehe 10 Mei, 2016. Kwa sasa huduma ya mabasi
katika kipindi cha mpito inatolewa katika njia nane, vituo vikuu vitano,
vituo vidogo 28 na karakana moja kwa kutumia mabasi 140 yanayojumuisha
mabasi makubwa 39 yenye uwezo wa kubeba abiria 160 kila moja na mabasi
madogo 101 yenye uwezo wa kubeba abiria 60 kila moja.
Mradi wa ujenzi wa Miundombinu ya
Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) umepangwa kutekelezwa kwa awamu sita kwa
lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Imetolewa na:
Eng. Joseph M. Nyamhanga
KATIBU MKUU (UJENZI)
24 Januari, 2017