Serikali Mkoani Simiyu imewashauri wakulima wote wilayani Busega wenye
mashamba yaliyo karibu na ziwa Victoria kuorodhesha jumla ya ekari za
mashamba waliyonayo ili waweze kusajiliwa na kuingizwa katika mpango wa kilimo cha umwagiliaji kinachotarajiwa kuanza mapema mwaka huu.
Ushauri
huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka katika ziara yake
maalum ya kuwatembelea wananchi wa vijiji vilivyopo kandokando ya ziwa Victoria Wilayani Busega, ambapo ameanza na vijiji vya Nyamikoma na Nyakaboja kata ya Kabita.
Mtaka alisema endapo wakulima watakuwa tayari kufanya kilimo cha umwagiliaji kwa
kufuata ushauri wa kitaalamu na kutumia mbegu bora watapata mazao mengi
yatakayokubalika katika soko la ndani na nje ya Mkoa ikiwa sambamba na na kujikwamua kiuchumi.
Alieleza kuwa lengo la serikali ya
Mkoa ni kuhakikisha dhana ya mapinduzi ya kilimo kwa mfumo wa
umwagiliaji inatekelezwa kwa vitendo kwa kuwapatia elimu ya kitaalamu
wakulima ili waweze kuzalisha mazao bora na mengi yanayotosheleza soko
la ndani ya nchi na kupunguza uagiziaji mazao nje ya Mkoa.
“Tumekuja
kama mkoa kuzungumza na wananchi ili wale watakaokuwa tayari waanze
kutekeleza. Ni lazima tufanye maamuzi ya kufanya mapinduzi ya kilimo
kama watu tulio kandokando ya ziwa Victoria ili uwepo ziwa utunufaishe”
amesema Mtaka.
Aidha alifafanua kuwa kilimo hicho katika maeneo ya Wilaya ya Busega kitahusisha
mazao ya Mpunga, mboga mboga, mahindi na mazao jamii ya mikunde, hivyo
wakulima kwa kushirikiana na Serikali wanatakiwa kuendelea kubuni mbinu mbalimbali
za uzalilishaji mazao hayo kwa wingi ili kwenda sambamba na fursa ya
masoko ya ndani na nje ya nchi hasa kwa mazao ya mikunde.
Mtaka
ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi imetoa
fedha katika Taasisi za fedha kwa ajili ya shughuli za kilimo, hivyo
akawashauri wananchi kujiunga katika vikundi ili iwe rahisi kuwatambua
na kuwawezesha kwa pembejeo na miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji
kulingana na makubaliano yatakayowekwa.
Hata
hivyo Mkuu huyo wa Mkoa amewasihi vijana nchini kujiajiri wenyewe
kupitia kilimo hicho kwa lengo la kupambana na changamoto ya ukosefu wa
ajira badala ya kukimbilia mijini wakati fursa za kujiajiri zipo nyingi
vijijini.
Kwa upande wake Mkulima wa kilimo cha mpunga Charles Malombo kutoka katika
kijiji cha Nyakaboja alisema licha ya serikali kuwa na mpango mzuri kwa
kuwapatia matumaini makubwa ya mafanikio katika kilimo cha umwagiliaji
bado wanahitaji msaada wa kitaalamu utakaowasaidia kutumia teknolojia ya
kisasa katika umwagiliaji maji ya ziwa Victoria ili waweze kupata mazao mengi zaidi ya wanayopata kwa sasa.
Naye
Samuel Chochomo ambaye ni Mkulima wa mazao mbali mbali ya Mboga mboga
alikiri kilimo hicho ndicho kitakachowatoa wakulima na wananchi katika
janga la njaa
Alieleza kuwa kilimo cha kutumia teknolojia ya umwagiliaji maji ni kizuri na hakitegemei
msimu wa mvua, wakulima wanaweza kulima wakati wote kama wakiwa na
miundombinu mizuri ya upatikanaji wa maji kutoka Ziwani na mipira imara
ya kusambazia maji.
Wilaya
ya Busega ni wilaya pekee Mkoani Simiyu iliyo na maji ya uhakika ya
Ziwa Victoria na eneo la takribani ekari 7200 zinazofaa kwa kilimo cha
umwagiliaji.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Kijiji
cha Nyakaboja wilayani Busega katika Mkutano wa hadhara kwa lengo la
kuwahamasisha kuanza kutekeleza mpango wa kilimo cha umwagiiaji wilayani
humo.
Mkuu
wa Wilaya ya Busega Tano Mwera akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha
Nyakaboja wilayani humo katika Mkutano wa hadhara kwa lengo la
kuwahamasisha wananchi kuanza kutekeleza mpango wa kilimo cha umwagiiaji
wilayani humo.
Afisa
Ardhi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Bibi.Grace Mgombera
akitoa ufafanuzi wa juu masuala ya ardhi yaliyowasilishwa na wananchi
wa Kijiji cha Nyamikoma B wilayani Busega kama kero kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka katika mkutano wa hadhara uliofanyik kjijini hapo.
Diwani
wa Kata ya Kabita wilayani Busega akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha
Nyakaboja wilayani humo katika Mkutano wa hadhara kwa lengo la
kuwahamasisha wananchi kuanza kutekeleza mpango wa kilimo cha umwagiiaji
wilayani humo.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa pili kulia) akisaini kitabu
mara baada ya kuwasili katika Kijiji cha Nyakiboja kata ya Kabita
wilayani Busega kabla ya kuwahutubia wananchi wa eneo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
Baadhi
ya Wananchi wa Kijiji cha Nyamikoma B Kata ya Kabita, wilayani Busega
wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika Mkutano
wa hadhara kuwahamasisha kuingia na kuanza kutekeleza mpango wa kilimo
cha umwagiiaji wilayani humo.
Baadhi
ya Maafisa wa Sekretarieti ya Mkoa walioambatana na Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika ziara yake ya kuwahamasisha wananchi wa
Busega kutekeleza mpango wa kilimo cha umwagiliaji.
Post a Comment