Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) inapenda kutoa ufafanuzi
kuhusu taarifa ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) iliyotolewa kwenye magazeti
ya Mwananchi na Uhuru ya tarehe 15/11/2017. Gazeti la Mwananchi liliandika,
“Serikali ‘yaiua’ rasmi TTCL na gazeti la Uhuru liliandika,“TTCL ‘bye’ ‘bye’.
Vichwa hivi vya habari vimewachanganya wasomaji na kuleta taharuki kwa wateja
na wafanyakazi wa TTCL, wadau wa Sekta ya Mawasiliano na wananchi kwa ujumla.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewasilisha Muswada wa
Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania katika mkutano wa Tisa wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 14 Novemba, 2017 mjini Dodoma. Bunge
lilijadili na kupitisha Muswada na kutungwa kuwa Sheria itakayoanzisha Shirika
la Mawasiliano Tanzania. Madhumuni ya Muswada yalikuwa ni kuanzisha Shirika la
Umma la Mawasiliano nchini kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi, kukuza uchumi
na kutoa huduma za mawasiliano kwa ubora unaotakiwa. Pia, kulipa Shirika la
Mawasiliano jukumu la kusimamia miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano nchini.
Sheria mpya
itaiwezesha TTCL kutekeleza majukumu yake kama Shirika la Mawasiliano nchini. Hizi
ni jitihada za Serikali kuimarisha TTCL na sio kuiua. TTCL bado ipo na
itaendelea kutekeleza majukumu yake kama Shirika la Mawailiano nchini. Shirika
litaendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa ubora na ufanisi zaidi.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
17 Novemba, 2017
Post a Comment