SERIKALI
ya Tanzania chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, imedhamiria
kuiimarisha Kampuni ya Simu nchini (TTCL) iIi iweze kuingia kwenye
ushindani wa kibiashara dhidi ya makampuni mengine ya simu.
Hayo
yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Waziri Kindamba
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya TTCL jijini
Dar es Salaam.
Kindamba
alisema hayo kufuatia Novemba 14, mwaka huu, Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kujadili na kupitisha miswada ya mapendekezo ya
mabadiliko ya sheria yanayofuta sheria iliyounda Kampuni ya Simu ya TTCL
(Tanzania Telecomunication Company, Incoporation Act 2002) na kutunga
sheria inayounda Shirika la Mawasiliano Tanzania (Tanzania
Telecommunication Corporation Act 2017).
Aliongeza
kuwa, kujadiliwa na kupitishwa kwa muswada huu bungeni kunafuatia hatua
za awali za miswada ya serikali ambapo maoni ya wananchi na wadau wa
huduma za mawasiliano yalikusanywa na kuchambuliwa.
Aidha,
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Kambi rasmi ya Upinzani
Bungeni zilichambua muswada huu na kuutolea mapendekezo yao, ambapo
Kindamba alisema mambo muhimu yanayotajwa katika sheria hiyo mpya ni
pamoja na; Kuweka utaratibu utakaowezesha TTCL kutekeleza majukumu yake
kama shirika la Umma. Kuweka jukumu la ujenzi, usimamizi na uendeshaji
wa miundombinu ya kimsingi ya Taifa, Kuweka mazingira ya kinga ya mali
(Asset) na miundombinu muhimu ya mawasiliano ya shirika na Kuanzishwa
kwa shirika na kuainisha uongozi wa shirika.
Mambo
mengine ni pamoja na Kuanisha vyanzo vya mapato na mtaji wa shirika,
Kuanisha sheria zingine zitakazoguswa, Sheria kutumika pande zote za
muungano na Kufuta kampuni ya simu Tanzania na kuanzisha shirika la
mwasiliano Tanzania.
Kindamba
aliongeza kuwa, katika mapendekezo ya sheria mpya yaliyoridhiwa na
Bunge, Shirika la Mawasiliano Tanzania linapewa jukumu la msingi la
kutoa huduma za mawasiliano kwa Taifa na kuhakikisha kuwa huduma hizo
zinatolewa kwa viwango vya juu vya ubora.
Aidha,
Kindamba alisema sheria mpya inataja jukumu jingine kuwa ni kusimamia
na kuendeleza miundombinu ya Ki-Mkakati ya Mawasiliano kama vile Mkonga
wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), Kituo Mahiri cha kutunzia kumbukumbu
(National Data Centre) na miundombinu mingine itakayokuja siku za usoni.
Awali
majukumu hayo yalikuwa yanafanywa na TTCL kwa niaba ya serikali bila
kutajwa katika sheria. Amesema, miongoni mwa upungufu ulioonekana katika
sheria ya awali ni kuwa, sheria hiyo ililenga kuwezesha mazingira ya
ubia ndani ya TTCL, hitaji ambalo sasa halipo tena kutokana na TTCL
kurejea mikononi mwa serikali kwa asilimia mia moja.
Kupitia
utaratibu huo wa ubia, kwa kipindi cha miaka 15, TTCL ilimilikiwa na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 65 na Kampuni
ya Bharti Airtel ya India kwa asilimia 35.
Kaimu
ofisa mtendaji huyo mkuu wa TTC L amesema, ubia huo ulifikia ukomo Juni
2016 baada ya Bharti Airtel ya India kulipwa jumla ya Tsh 14.7 Bilioni
na kuondoka ndani ya TTCL.
Kindamba
amesema hoja mahususi ni kwamba Shirika la Mwasiliano ni chombo muhimu
katika ustawi wa nchi na kuongeza kuwa sheria mpya itaongeza ufanisi na
tija katika shirika hilo ili liweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya
Watanzania wote.
“TTCL
ni taasisi yenye hazina kubwa ya watendaji wenye weledi na uzoefu
mkubwa wa shughuli za mawasiliano hapa nchini,” alisema Kindamba na
kuongeza; TTCL imeonesha weledi na uzoefu mkubwa katika kusimamia na
kuendesha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye mtandao wa takriban
kilomita elfu saba na mia nne nchi nzima.
Aidha,
Kindamba amesema TTCL inasimamia na kuendesha kwa ufanisi mkubwa kituo
mahiri cha kuhifadhi kumbukumbu (National Data Centre) kinachohudumia
taasisi 28, taasisi 19 za serikali na taasisi 8 za sekta binafsi hadi
sasa. “Makampuni yote ya mawasiliano na wadau mbalimbali wa biashara
wanaotumia huduma zaTTCL wanaridhika sana na huduma inayotolewa,”
alisema Kindamba na kuongeza;
“Kuhusu
kuipa mtaji TTCL, serikali imeandaa mpango mkakati wa miaka mitano
2017/18-2021/2022 ambao pamoja na mambo mengine utaainisha mtaji
unaohitajika na serikali ambapo serikali itatekeleza mpango huo.”
Aliongeza
kuwa, kuhusu idadi ya wajumbe wa bodi kutoka Zanzibar, serikali
imeridhia idadi hiyo kuongezeka kutoka mjumbe mmoja na kuwa wawili.
Kindamba
amesema ieleweke kwamba mabadiliko haya ya sheria kutoka Kampuni ya
Simu Tanzania kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania hayaathiri mikataba
na makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa awali kati ya TTCL na wateja
na wadau wa huduma zake.
Amesema
madeni ambayo TTCL inadai wateja wake na ambayo TTCL inadaiwa na watoa
huduma mbalimbali yapo palepale na yataendelea kufanyiwa kazi kwa mujibu
wa makubaliano na mikataba ya kiabishara iliyofikiwa.
“TTCL
ipo imara na thabiti zaidi kuliko ilivyokuwa awali kwa kuwa sasa
inatarajia kupata mamlaka zaidi na uwezo zaidi wa kuhudumia umma,”
alisema Kindamba.
Akielezea
mustakabali wa ajira za wafanyakazi wa kampuni hiyo baada ya mabadiliko
hayo, Kindamba amesema ajira zao ikiwa ni pamoja na mali na
miuondombinu viko salama.
Kindamba
amesema huduma zinazotolewa na TTCL yaani simu za mezani, simu za
kiganjani, data na TTCL PESA zinaendelea kutolewa kwa ufanisi mkubwa na
kuongeza kuwa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo
mahiri cha kutunzia kumbukumbu (National Data Centre) pia zinaendelea
kutolewa kama kawaida na kwa weledi wa hali ya juu.
“Kilichobadilika
ni sheria ya kampuni ya simu Tanzania ambayo sasa ni shirika la
mawasiliano Tanzania ambapo mapendekezo haya yanasubiri idhini ya
mheshimiwa rais ili kuwa sheria kamili,” amehitimisha Kindamba.
Post a Comment