Imeelezwa kuwa
kutungwa kwa sheria ya kulinda taarifa binafsi kutapunguza uhalifu
unaohatarisha amani na kuongeza usalama wa mtu, jamii, nchi na dunia kwa
ujumla.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Maria Sasabo, amesema
hayo katika kikao cha wadau cha kupitia mapendekezo ya kutungwa kwa sheria ya
kulinda taarifa binafsi na kusisitiza umuhimu wa kujielimisha kabla ya
kusambaza taarifa.
“Ni muhimu kwa jamii
kuelewa haki ya faragha ya mtumiaji wa mawasiliano na namna ya kushughulikia
taarifa katika ukusanyaji, usambazaji, uchakataji na uhifadhi ili kuepuka
kutenda uhalifu” amesema Dkt. Sasabo.
Dkt. Sasabo
amezungumzia umuhimu wa jamii kuzingatia sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka
2015 na sheria ya miamala ya kielektroniki ya mwaka 2015 ili kuepuka makosa
yasiyo yalazima na kuepuka usambazaji wa taarifa binafsi za watumiaji wa
mawasiliano usiouwiana na maadili na wenye nia ovu.
“Ni vema jamii ikajua
mitandao haina mipaka, hivyo ni muhimu kuwa na muongozo utakaosimamia haki za
watumiaji na kulinda taarifa binafsi”, amesisitiza Dkt. Sasabo.
Naye, Afisa Sheria wa
Sekta ya Mawasiliano, Bi. Eunice Masigati, amesema mabadiliko ya sayansi na
teknolojia yamechangia ongezeko kubwa la makosa katika mawasiliano ya simu na
intaneti hivyo uwepo wa sheria inayosimamia taarifa binafsi utapunguza
changamoto za kimtandao na kuongeza haki ya faragha.
Dkt. Sasabo, alikuwa
katika kikao kazi cha wadau kukusanya maoni ya mapendekezo ya kutungwa sheria
ya kulinda taarifa za watumiaji ili kupunguza uhalifu na kuhakikisha usalama wa
taarifa binafsi.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
Post a Comment