Mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis anayekabiliwa na makosa ya rushwa ameachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.
Sadifa ameachiwa leo Desemba 19, 2017, na Mahakama ya Mkazi Dodoma baada ya kukosa dhamana wiki iliyopita kutokana na upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kiapo kuzuia dhamana kwa madai kuwa angevuruga upelelezi na kuingilia uchaguzi wa UVCCM uliofanyika Desemba 10 – 11, 2017, mjini Dodoma.
Mahakama leo imetupilia mbali pingamizi hilo na kutoa masharti ya dhamana kwamba Sadifa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh1 milioni na wenye vitambulisho vinavyotambuliwa na mamlaka ya maeneo wanakoishi. Huku Sadifa akitakiwa kutotoka nje ya mipaka ya nchi bila kibali cha Mahakama na kesi yake itatajwa mwakani Januari 18.
Awali Sadifa alipofikishwa mahakamani na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Biswalo Biswalo alidai kuwa Sadifa anashtakiwa kwa makosa mawili ya kutoa rushwa katika mazingira mawili tofauti tofauti kwa siku moja.
Ambapo alieleza kuwa mtuhumiwa mnamo Desemba 9,2017 katika Kata ya Mnada mjini Dodoma akiwa mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM aliwahonga wanachama ili wamchague Rashid Mohamed aliyekuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi mkuu wa umoja huo.
Katika tukio la pili mshtakiwa anadaiwa katika eneo hilo na siku hiyohiyo, aliwaahidi kuwalipia usafiri wanachama wa umoja huo kuwasafirisha kutoka Dodoma hadi Kagera kama zawadi ili wamchague Rashid Mohamed.
Mwisho.
Post a Comment