Na David Nyembe, Chunya
MKUU wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Maryprisca Mahundi,
amewapa wiki tatu wafugaji wa Kijiji cha Igundu katika Kata ya Sangambi
wilayani humo kuhamisha mifugo yao na kuipeleka katika Kijiji cha Paris ambacho
kimetengwa kwa ajili ya wafugaji.
Ametoa kauli hiyo wakati wa Mkutano wa Hadhara uliofanyika
kijijini hapo ambapo alisema lengo la kuondoa mifugo hiyo ni kumaliza mgogoro
kati ya wakulima wa kijiji hicho na wafugaji pamoja na kuokoa chanzo cha maji
ambacho wakazi wa eneo hilo wanakitegemea.
Alimuagiza Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Joseph Nangale,
kusimamia na kuhakikisha mifugo hiyo inahamishwa huku akimtaka kutumia nguvu
iliyotumika kuwazuia wakulima kufanya shughuli zao karibu na chanzo cha maji.
Mahundi alisema amechoshwa na migogoro ya wakulima na
wafugaji katika kijji hicho cha Igundu na kwamba agizo lake hilo ni la mwisho
na kwamba atakaporudi tena kwenye kijiji hicho na kukuta inaendelea hakutakuwa
na majadiliano tena na kwamba wasije wakamlaumu.
“Mkae chini mjadiliane na mkubaliane idadi ya mifugo ambayo
kila mfugaji wa kijiji hiki atatakiwa kubaki nayo hapa, nimewapa siku 10
viongozi wenu waniletee taarifa ya majidiriano hayo, lakini nimewashauri kila
mfugaji abaki na mifugo 10,” alisema Mahundi.
Alisema idadi hiyo aliyopendekeza kila mfugaji abaki nayo
kijijini hapo ni rahisi kuimudu ili isiingie kwenye mazao ya wakulima na kwamba
itasaidia kumaliza migogoro.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Nangale alikiri kijiji hocho
kuwa na idadi kubwa ya mifugo kuliko uwezo wa eneo la kijiji hicho hali ambayo
inapelekea migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji.
Alisema migogoro hiyo ilikuwa inaibuka baada ya mifugo
kuwashinda wafugaji na kuingia kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao na
hivyo kuwafanya wakulima waanze kutaka kulipiza kisasi.
Aliahidi kushiriiana na halmashauri nzima ya kijiji hicho
katika kutekeleza agizo la Mkuu wa Wilaya la kuondoa mifugo na kwamba
watayashirikisha makundi yote ili kufikia mwafaka ambao hautaleta shida.
“Kijiji cha paris kina eneo kubwa kwa ajili ya mifugo na ni
eneo rafiki kwa sababu hakuna mwingiliano na shughuli zingine za kibinadamu,
tulikitenga maalumu kwa ajili ya wafugaji,” alisema Nangale.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya aliwatahadharisha
viongozi wa vijiji wanaopokea rushwa kutoka kwa wafugaji ili waingize mifugo
kwenye vijiji vyao kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria endapo
watabainika.
.
Mwisho.
Its a very great article, really unique content thank you !
ReplyDeletetrickcode
sarkari Yojana