Na EmanuelMadafa,Mbeya
POLISI Mkoani Mbeya, imelazimika
kutumia mabomu ya machozi na maji ya washawasha katika kuwatawanya madereva
pikipiki(Boda Boda) wa Jiji la Mbeya, ambao walimzingira mshukiwa wa mauji ya
dereva mwenzao aliyeuawa April 8, mwaka huu kwa nia ya kumuua.
Marehemu Siza
Mwambenja(28) Mkazi wa Airpot jijini Mbeya aliuawa na watu wasiojulikana
na kisha mwili wake kutupwa kwenye pori lililopo eneo la Senjele.
Kwa mujibu wa Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakael Masaki amesema marehemu huyo alipotea
katika mazingira ya kutatanisha April 8 mwaka huu akiwa na pikipiki yake
yenye namba za usajili T.932 CTZ akiwa na mteja ambaye hakufahamika jina
lake.
Amesema, askari polisi
wakiwa katika harakati za kumtafuta mtuhumiwa walipata taarifa ya kwamba dereva
bodaboda hao wamekuwasanyika na wanaelekea kwenye nyumba ya marehemu kwa lengo
la kumkamata mwanamke huyo huku wakiwa na nia ya kumuua.
Inadai kuwa madereva hao
kabla ya kuelekea kwenye nyumba ya marehemu walifanikiwa kumkamata
shemeji wa marehemu ambaye hawakumtaja jina na walipombana ndipo inadaiwa
alikiri yeye na dada yake walihusika na mauji ya shemeji yake.
Wakati wakiwa kwenye
mahojiano hayo shemeji huyo alifanikiwa kuwatoroka hivyo na wao kuanza
kumtafuta na kupata taarifa ya kwamba mke wa marehemu yupo nyumbani kwake.
Madereva hao wakiwa
kwenye vyombo vyao vya usafiri walifika kwenye nyumba ya
marehemu na inadaiwa kuwa mara tu baada ya mama huyo
alipouona msafara huo alikimbilia ndani na kujifungia.
“Sisi lengo letu la
kufika kwenye nyumba hii ni kumkamata muuji wetu na kumpa adhabu ya kifo kama
aliyompatia mwenzetu hivyo tutavunja nyumba hii na kumtoa ndani,”alisema dereva
bodaboda ambaye hakutaka jina lake liandikwe.
Wakati wakiwa kwenye
harakati za kuvunja nyumba hiyo ndipo askari polisi walipofika na kufanikiwa
kuusambaratisha msafara huo kwa kutumia mabomu na maji ya washawasha huku
baadhi yao ambao walionekana kushindwa kutii sheria waliambulia kipigo.
Askari, walifanikiwa
kumuokoa mwanamke huyo na kwenda kumuhifadhi polisi huku wakiendelea na
harakati za kumtafuta shemeji wa marehemu ambaye inasemekana alikimbia.
Akielezea tukio hilo
Mwenyekiti wa madereva bodaboda, Vicenti Mwashoma, ameutupia lawama uongozi wa
polisi kwamba ndio chanzo cha vurugu hizo.
“Jeshi lilipaswa
kushirikisa viongozi badala ya kuanza kutumia nguvu kubwa ambayo
imesababisha uharibifu mkubwa wa mali za watu pamoja na baadhi
kujeruhiwa,”alisema.
Mwisho.
Post a Comment