MBEYA CITY
COUNCIL FOOTBALL CLUB
TAARIFA KWA
UMMA NA.02
Maamuzi mabaya
katika mchezo wetu dhidi ya Azam Fc
Klabu inachukua
nafasi hii kuujulisha umma namna inavyosikitishwa na baadhi ya matukio
yanayoendelea kujitokeza katika baadhi ya michezo ya ligi kuu Tanzania
inayokamilika tarehe 19/04/2014.
Katika mchezo
huo wa tarehe 13/4/2014 uliochezwa uwanja wa sokoine jijini Mbeya tulishuhudia
timu yetu ikichezeshwa vibaya sana na waamuzi wa mchezo husika,Waamuzi hao ni
muamuzi wa kati Nathani Lazaro(Kilimanjaro),Abdallah Uhako AR1(Arusha) na
Godfrey Kihwil AR2 (Arusha). Waamuzi hawa kwa makusudi waliamua kuuharibu mchezo
huo kwa kufanya maamuzi mengi mabaya na yenye utata kwa maslahi ya timu pinzani
yetu siku hiyo.
Baada ya mchezo
husika klabu ilitengeneza jopo la watalaam wa sheria na taratibu zinazosimamia
mchezo wa soka ili waishauri kwa kile kilichoonekana siku ya mchezo huo
kuhusiana na tafsiri ya sheria za mchezo toka kwa waamuzi hao. Kwa ufupi
tunasema hivi:
- Nidhamu ndani na nje ya uwanja ni msingi wetu mkuu na tumekuwa tukisimamia muda wote,kwa upande wetu nidhamu si swala la kufundishwa wala kukumbushwa na mtu,kwa namna muamuzi alivyoanza kuwatoa mchezoni kisaikolijia wachezaji wetu kwa maneno hasa katika kipindi cha kwanza hakuwa na nia njema na mchezo wetu siku hiyo,wakati wa kuelekea mapumziko wachezaji wetu walimshihi aamue kwa haki ili asiwe sababu ya kuharibu mchezo huo.Haijawah kutokea kama timu kumzonga muamuzi yeyote yule lakini kwa makusudi waamuzi wa mchezo husika walitengeneza mazingira ya kutufikisha hapo.
- Utata wa penati,mchezaji wa Azam Fc alimuongopea muamuzi kuwa kafanyiwa madhambi ndani ya eneo la mita kumi na nane la gori la Mbeya City,muamuzi wa katikati aliiona fika sehemu sahihi ambako kosa lilifanyika lakini kwa dhamila yake mbaya akikimbia toka katikati ya uwanja alikwenda huku akiashiria kuwa ile ni penati wakati muamuzi msaidizi akiwa haoneshi hivyo,baada ya wachezaji wetu kugomea adhabu ya penati kwa mshangao muamuzi wa kati alibadirisha hata eneo stahili la adhabu ilipopaswa kupigwa.
- Utata wa goli la pili la Azam Fc,Hapa ndipo fumbo kubwa lilipodhihirika,mchezaji wa Azam Fc alifnya madhambi kwa kucheza vibaya na hivyo muamuzi msaidizi aliona na kuonesha kibendera juu,bado mchezaji wa Azam fc aliukuta mpira baada ya yeye kucheza vibaya dhidi ya mchezaji wetu,huku bado muamuzi msaidizi akiwa amenyoosha kibendera juu mchezaji huyo alifunga goli huku muamuzi wa kati akiona yote hayo, yeye muamuzi wa kati aliamulu hilo ni goli wakati muamuzi wa pembeni hakuashiria hivyo.Hapa napo ndipo sintofahamu kubwa ilipotokea.Goli hili lilikuwa la dhuluma.
- Kwa ujumla waamuzi hawakuumudu mchezo kwa makusudi.
Klabu haiamini kuwa waamuzi hawa hawakuwa
na uwezo ama sifa za kuchezesha mchezo ule,kama ingekuwa hivyo wasingeweza
kufuzu katika majaribio mbalimbali ya kuwa na sifa za kuchezesha ligi kuu ila
tunapata hisia kuwa waamuzi hawa walighiribiwa ili wachezeshe kwa faida
ya wapinzani wetu.
Matukio ya aina hii yanaweza kuhatarisha
amani katika viwanja vyetu,na kuupa tafsiri mbaya mchezo wa mpira wa miguu
wenye wapenzi wengi waungwana.Hakuna jambo ambalo ni jema litokanalo na
uhalifu,kama mamlaka husika nazo zitabaki kusema “huo ndio mpira wetu”
basi mpira kwetu hautakuwa na maana.
Wapanga matokeo ni hatari kwa mpira wetu.
Wizi wa mapato ya milangoni
Kwa mara nyingine klabu imeshuhudia wizi
mkubwa wa mapato ya milangoni,baada ya kupata matatizo kama haya katika mechi
dhidi ya Mtibwa Sugar na Simba zilizochezwa Mbeya wakati wa mchezo dhidi ya
Azam Fc tatizo hilo limejirudia tena.
Maandalizi ya tiketi yalifanyika vizuri
lakini hadithi ya kuwa vitabu vilisahaulika kugongwa mihuri imejirudia tena,Si
kweli kuwa vitabu vilisahaulka lakini klabu inapata hisia kuwa mchezo huu
umeota mizizi na kuna watu wanaouratibu sambasamba na mfumo halali kwani risiti
hizi ambazo hazikuwa na mhuri wa klabu ziliuzwa ndani ya mfumo wa uuzaji tiketi
halali.
Klabu ilibaini vitabu vifuatavyo
havikugongwa mihuri na viliuzwa ndani ya mfumo ulio halali zikiuzwa na wauzaji
maarufu wa tiketi wa kila mechi ichezwayo Mbeya,Vitabu hivyo ni namba 06700,08700,11100,12800,13500
na 16600.Hivi ni vile ambavyo tuliweza kuviona hatuna hakika ni vingapi
havikuonekana ambavyo tayari viliuzwa kama vilivyouzwa hivi.Pamoja na kuripoti
suala hili kwa mafias wasimamizi wa kituo hakukuwa na dalili zozote za kushtushwa
na hili.
Tumechoshwa na hali hii isiyokuwa na
huruma kwa mapato madogo ya wachezaji wenye kipato kidogo.Tusipokuwa na dhamila
ya dhati ya kuwadhibiti watu wenye njaa isiyokoma waliopo kwenye mpira wetu
tutakuwa tunatengeneza baadhi ya timu ziitumikie timu zingine hivyo kuondosha
dhana ya ushindani iliyojengeka msimu huu.Fedha itokanayo na mapato halali kama
ya milangoni ni muhimu katika ujenzi wa timu imara na zenye ushindani ambazo
zitaimarisha ligi yetu na hatimaye timu ya taifa imara,kuendelea kuufumbia
macho wizi kama huu wa mapato ya milangoni ni kukaribisha maafa makubwa katika
mpira wetu.
Wizi kama huu hauwezi kufanywa na watu
baki zaidi ya wale wanaojua utaratibu mzima wa uandaaji na uratibu wa
tiketi hizi.
Freddy.Jackson
AFISA HABARI
MCC FC
18.04.2014
Post a Comment