Pichani Mkuu wa Wilaya ya Kyela aliyesimama Ndugu Esthar Malenga picha na Maktaba |
Na Mwandishi wetu,Kyela
ZAIDI ya Wananchi
100,000 wilayani Kyela mkoani Mbeya wapo hatarini kukumbwa na magonjwa ya
mlipuko kutokana na kutumia maji yasiyofaa kwa afya za binadamu kufuatia visima
vyao vya awali kuharibiwa na mafuriko yaliyotokea wilayani humo April 12 mwaka
huu.
Hatari hiyo inatokana na wananchi
hao sasa kulazimika kutumia maji yaliyotuama kwenye maeneo yao baada ya kutokea
kwa mafuriko hayo kwa ajili ya kunywa na kupikia vyakula
Mkuu wa Wilaya ya Kyela,
Margret-Esther Malenga, amesema kati ya kata 20 zilizomo wilayani humo, kata 12
wananchi wake bado wamezingirwa na maji hivyo wanalazimika kutumia maji yasiyo
salama kwa ajili ya kujikimu kwa maisha yao ya kila siku.
Malenga ametoa taarifa hiyo wilayani
humo wakati akipokea msaada ya dawa za binadamu kutoka kwa Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya, NHIF, ili kukabiliana na magonjwa yatakayotokana na mafuriko
hayo.
Wilaya ya Kyela ina zaidi ya wakazi
225,000, Malenga, amesema takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya nusu ya wakazi hao
wanakabiliwa na hatari ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na kutumia
maji hayo.
Kibaya zaidi, Malenga amesema licha
ya Wataalam wa wilaya hiyo kuwaelimisha wananchi hao kuchemsha maji hayo ili
kujiepusha na magonjwa lakini bado wanakabiliwa na wakati mgumu wa kutekeleza
ushauri huo kutokana na kwamba hakuna kuni za uhakika kufuatia miti yote kubaki
majini.
Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Festo
Dugange amesema tayari wameanza kuchukua tahadhari ya kuhakikisha wanakuwa na
dawa za kutosha endapo mlipuko huo wa magonjwa utajitokeza pamoja na kutoa
elimu kwa wananchi hao kuhusu umuhimu wa kuchemsha maji ya kunywa.
Meneja wa NHIF Kanda ya Nyanda za
Juu Kusini, Mohammed Kilolile, amesema mfuko huo utaendelea keshirikiana na
Serikali wilayani humo ili kuhakikisha uthibiti wa kutosha wa magonjwa hayo
endapo yatatokea.
Jumla ya kaya 3,983 zimeathiriwa na
mafuriko hayo wilayani Kyela na kusababisha watu kadhaa kukosa makazi.
Post a Comment