Mtuhumiwa akitoka mahakamani |
Na EmanuelMadafa,Mbeya
MAHAKAMA ya hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Mbarali imemuachia huru
mwalimu wa shule ya sekondari Montfort inayomilikiwa na kanisa Katoliki la
mjini Rujewa, Andrea Shadrack, aliyekuwa anakabiliwa na tuhuma za kubaka
wanafunzi watatu.
Shadrack ambaye ni ‘Bruda’ wa kanisa la
Katoliki kigango cha Iringa alifikishwa mahakamani hapo baada ya kutenda kosa
hilo Septemba 12 mwaka 2013 majira ya saa 3:30 ndani ya eneo la shule.
Hukumu iliyomwachia huru Mwalimu Shadrack,
ilitolewa juzi na hakimu Mkazi Mfawidhi, Kinabo Minja, baada ya upande wa
mashitaka kushindwa kuthibitisha kutendeka kwa tukio hilo.
Ambapo vielelelezo kutoka jeshi la polisi,
ambavyo ni fomu namba tatu ya polisi (PF3) ambavyo hutolewa kwa mlalamikaji ili
aweze kupatiwa matibabu kuonekana kuwa na utata.
Akisoma uchambuzi wa ushahidi hakimu Minja
alisema wasiwasi wa vielelezo hivyo ni kutofautiana kwa tarehe, pamoja na
majibu ya uchunguzi wa daktari kuonekana
kupishana kwa wino, kufutwa futwa na maandishi yake kuonekana kufifia.
Mara baada ya hukumu hiyo Mwalimu Shadrack
alionekana kububujikwa na machozi ambapo alipokelewa na mwenzake na kuondoka
haraka sana eneo hilo la mahakama, huku upande walalamikaji ukishikwa na butwaa.
Hakimu Minja,alisema ni jukumu la mahakama
kuthibitisha mshitakiwa anahatia na kwamba mambo makuu yaliyoangaliwa kwenye
kesi hiyo ambayo ni kinyume cha sheria namba 130/131 sura ya 16 ya mwaka 2002
ni kuthibitisha uwepo wa tendo la ngono pamoja na kutokuwepo kwa ridhaa.
Hata hivyo, amesema katika kupitia maelezo ya
pande zote mbili, mahakama imebaini kuwepo kwa tendo la ngono kutokana na
taarifa zilizotolewa na madaktari walio wafanyia uchunguzi wanafunzi hao na
kuthibitisha ya kwamba walikuwa na michubuko.
Aidha, amesema mahakama pia iliridhika na
ushahidi uliotolewa na wanafunzi hao ya kwamba Mwalimu huyo aliwaingilia
kimapenzi pasipo idhini yao na kwamba alitumia vitisho kwa kuwataka wasiseme
kwa mtu yoyote mara alipomaliza kufanya kitendo hicho.
Amesema katika kuchambua na kupitia vielelezo
vilivyotolewa na polisi ambazo ni fomu namba tatu vilionekana kuwa na utata
mkubwa, kwani zilitolewa katika vituo viwili tofauti vya polisi.
Amesema katika fomu ya mlalamikaji namba moja
malalamiko yalitolewa kituo cha polisi Rujewa Septemba 14 , wakati walalamikaji
namba mbili na tatu maelezo yao yalitolewa kituo cha polisi Mbarali Septemba 13.
Kutokana na hali hiyo, mwendesha mashitaka wa
polisi, Mazoya Luchagula, aliweka wazi kutoridhishwa na maamuzi hayo na kwamba
unatarajia kukata rufaa ili hukumu hiyo ipitiwe upya.
Mwisho.
Post a Comment