Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This






 Na EmanuelMadafa,Mbeya
KATIBU Mkuu Ikulu, Peter Ilomo, amewataka watendaji wa Sekratieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuzingatia maadili ya kazi yao kwa kutunza siri za sekretarieti hiyo kuhusu taarifa mbalimbali za viongozi wanaoshughulikiwa na chombo hicho.



Ilomo, alitoa changamoto hiyo, wakati akifungua Mkutano wa 12 wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma unaofanyika kwa siku mbili Jijini Mbeya.


 Amesema, changamoto kubwa inayoikabili sekretarieti hiyo ni namna ya utunzaji wa siri za viongozi  mbalimbali 
wanaochunguzwa na mamlaka hiyo katika utendaji kazi wake wa kawaida hivyo wakati umefika kwa watendaji  kuhakikisha wanazingatia maadili yao ili kukifanya chombo hicho kuaminika kwa wananchi.

Ilomo amesema Sekretarieti hiyo inautaratibu wa kukusanya na kutoa taarifa za viongozi wanaofanyiwa kazi hivyo watendaji hao wanapaswa kuzingatia utaratibu huo ambao ni sehemu ya maadili yao.

Awali akimkaribisha Ilomo kufungua mkutano huo, Kamishna wa Maadili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Salome Kaganda, amesema licha ya majukumu makubwa ya sekretarieti hiyo lakini bado inakabiliwa na upungufu wa watumishi na hivyo kuiweka katika wakati mgumu kiutendaji.


Kaganda, amesema hadi sasa Tanzania ina viongozi 13,167 wanaofuatiliwa na sekretarieti hiyo lakini mamlaka hiyo ina watumishi 200 hivyo kukosekana kwa uwiano mzuri kiutendaji.


Pia Kaganda, amesema bado suala la mgongano wa kimaslahi ni changamoto nyingine kwa sekretarieti hiyo kutokana na baadhi ya viongozi kumiliki biashara zinazopaswa kukaguliwa huku wenyewe wakiwa hawapo tayari kusema ukweli kuhusu umiliki wa mali hizo.



Mkutano huo wa siku mbili unawahusisha viongozi wa sekretarieti hiyo kutoka  kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, Kanda ya Ziwa inayoundwa na mikoa ya Mwanza, Geita, Mara na Kagera, Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Tabora, Kigoma, Simiyu na Shinyanga, Kanda ya ya Kati mikoa ya Dodoma na Singida, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Katavi na Rukwa, kanda ya Kusini mikoa ya Lindi, Mtwara  na Ruvuma huku Kanda ya Mashariki ikiwa na mikoa ya Tanga, Morogoro na Pwani.


Mwisho

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top