Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Baadhi ya Watuhumiwa kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu Teku wakifikishwa Mahakamani ambao  ni pamoja na Askari F 5842 DC Maduhu watatu kutoka juu  na WP 6545 DC Neema wa kwanza kutoka juu aliyejifunika na mtandio wakiwa pamoja na ndugu zao . 
Ndugu  wa askari Neema wakijaribu kumficha mtuhumiwa huyo ili asibambwe na kimulimuli chetu
watuhumiwa wakirudishwa rumande
Na EmanuelMadafa.Mbeya

MAHAKAMA  Kuu  ya Tanzania(Mbeya), imeanza kusikiliza kesi ya waliokuwa askari polisi watatu ambao wanadaiwa kuhusika na  mauaji ya aliyekuwa  mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Teofile Kisanji (TEKU)  Daniel Mwakyusa.

Waliofikishwa Mahakamani mbele ya Jaji Temba kwa kesi namba 26/2013 ni pamoja na Askari F 5842 DC Maduhu,F 7769 DC Shaban na WP 6545 DC Neema ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea Mika Thadayo Mbise.

Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Hashim Ngole, aliiambia Mahakama hiyo, watuhumiwa wote kwa pamoja walihusika na mauaji ya Daniel Mwakyusa February 14 mwaka 2012 ambapo watuhumiwa wanadaiwa kumpiga marehemu huyo kwa kutumia silaha inayodhaniwa kuwa ni bunduki   nje ya ukumbi wa starehe ujulikanao Univesal uliopo Uyole jijini Mbeya.
          
Aidha, watuhumiwa wote walikana mashitaka yao, ndipo wakili upande wa serikali  alianza kuwaongoza mashahidi watano kutoa ushahidi mahakamani hapo chini ya kiapo huku Jaji akisaidiwa na wazee watatu wa Baraza  ambao ni Agry Ngao,Sheria Mwakatumbula na Pilly Mwakatundu.

Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo alikua ni Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu huyo kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya Dkt.Yunusi Mbaga, ambaye aliimbia mahakama kuwa kifo cha marehemu kilitokana na kuvuja damu kwa wingi katika mapafu na moyo wake.

Amesema, kuvuja kwa damu huko kulitokana na majeraha yanayodhaniwa kuwa ni ya risasi ingawa katika uchunguzi baada ya upasuaji mwili wa marehemu hakukutwa na risasi yoyote licha ya kuwepo kwa uthibitisho wa  matundu sita ya risasi kwenye mwili wake.

Akitoa ushahidi wake shahidi wa pili ambaye alikua ni muuguzi wa zamu katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambaye  alijitambulisha kwa jina la  Sivian, alisema yeye aliupokea mwili wa marehemu Daniel February 14 mwaka 2012 usiku na kuuhifadhi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Akielezea utaratibu wa hospitali wa kupokea miili ya marehemu, Muuguzi huyo alisema muuguzi wa zamu anapaswa kupokea maiti usiku kutoka kwa askari polisi kwa kuzingatia taratibu husika ikiwemo ya wahusika ambao watahusika na mwili huo kujaza fomu husika lakini kwa siku hiyo jambo hilo halikufanyika.


Muuguzi huyo, aliendelea kufafanua kuwa yeye akiwa amemaliza kuhifadhi mwili huo na kukifunga chumba hicho, matumaini yake yalikuwa ni kuwakuta askari hao nje wakisubiri kujaza fomu hiyo lakini cha ajabu wakati akitoka nje alishangaa kutowaona wahusika hao.


Kwa upande wake shahidi wa tatu, ambaye ni mfungwa katika Gereza la Ruanda lililopo Mkoani Mbeya, Otieno Edward, ambaye aliimbia mahakama ya kuwa siku ya tukio yeye alikuwa ni mlinzi wa kumbi hiyo ya starehe na kueleza jinsi ya tukio lilivyotokea.

Mbali na hilo shahidi huyo alitumia nafasi hiyo kuiambia mahakama ya kwamba kutokana na  yeye kuwa shahidi katika kesi hiyo, jeshi la polisi limembambikia kesi ya  wizi wa kutumia silaha hali iliyopelekea kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.


Baada ya kusikiliza malalamiko ya shahidi huyo Jaji, alimwagiza Wakili wa serikali kufuatilia suala na kupatiwa  ufumbuzi haraka iwezekanavyo.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mahakamani hapo   na kwamba Shauri hilo limevuta hisia za watu wengi na kufanya ukumbi wa Mahakama kuu kufurika mahakamani hapo.
 Mwisho


Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top