Kamanda wa Polisi Mbeya Ahmed Msangi |
Na Mwandishi wetu,Mbeya
WATU sita wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wakiwa na silaha
wamevamia nyumba ya kulala wageni iliyopo Wilayani Momba Mkoani Mbeya na
kufanikiwa kuondoka na kiasi cha fedha cha shilingi 1,800,000 na kumjeruhi mtu
mmoja kwa risasi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema tukio
hilo limetokea jana, majira ya saa nne usiku katika mtaa wa Mwaka Tarafa
ya Tunduma Wilayani Momba Mkoani Mbeya.
Amesema, watu hao wanaodhaniwa ni majambazi wakiwa na silaha aina
ya Short Gun, walivamia katika Bar na nyumba ya kulala wageni iitwayo
"Feel Hapy" na kumjeruhi kwa risasi Simon Enock(42) katika mguu wake
wa kulia.
Aidha, Kamanda Msangi alisema, mbali na majambazi hao
kuondoka na kiasi hicho cha fedha pia waliondoka na mauzo ya siku hiyo ambayo
kiasi chake hakikuweza kufahamika.
Hata hivyo, amesema kuwa askari polisi walifanikiwa kuwatia
nguvuni baadhi ya watuhumiwa na kwamba wengine wanatafutwa kutokana na
kufanikiwa kukimbia mara baada ya kufanya tukio hilo.
Katika tukio lingine, Polisi Mkoani Mbeya, wamefanikiwa kukamata
risasi 40 za Bastola baada ya kufanya upekuzi katika moja ya nyumba ya kulala
wageni iitwayo “Sogea Tours Hotel&Guest House” iliyopo mtaa wa Sogea-
Tunduma Wilayani Momba Mkoani Mbeya.
Akielezea tukio hilo, Kamanda Msangi, alisema risasi hizo
zilikutwa ndani ya chumba kimoja ambacho inasemekana kuwa tangu kikodiwe
hakijawahi kufunguliwa na aliyekikodi hayupo.
Amesema, upekuzi ulivyofanyika risasi hizo zilikutwa zikiwa
zimehifadhiwa katika mfuko wa plastic(Rambo) na kuwekwa kwenye kasha lake na
kisha kuwekwa chini kwenye begi lililokutwa chumbani humo.
Post a Comment