Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
 
Na Mwandishi wetu,Rungwe
MPANGO wa kuiingiza Kata ya Kyimo kuwa sehemu ya mji wa Tukuyu wilayani Rungwe umestukiwa na wananchi wa Kata hiyo ambao wamedai kuwa wamebaini mbinu chafu za Mkuu wa Wilaya hiyo Chrispne Meela, kutaka kujinufaisha yeye binafsi.
 
Wananchi hao wanamtuhumu Meela kuwa ameshirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kukopa fedha katika benki moja kubwa nchini na sasa wanataka kuchukua mashamba yao ya chai kwa ajili ya kuyapima viwanja na kuviuza kwa matajiri ili waweze kulipa deni hilo.
 
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama cha Jamii Tanzania (Mujata) kwa lengo la kusuluhisha mgogoro huo wa ardhi, wananchi hao wamesema hawako tayari kuona mashamba yao ya chai yakigawanywa vipande vidogovidogo na kuuzwa kwa matajiri bila ya ridhaa yao.
 
Akisoma risala ya wananchi hao mbele ya viongozi wa Mujata, Hassan Mwandetele alisema kuwa wanaopinga mpango huo ni wananchi wengi wa kata hiyo ambao wanahofu mashamba yao ya chai na mazao mengine kuchukuliwa bila ridhaa yao na kuingizwa kwenye mpango huo.
 
“Hatuko tayari kuona mashamba yetu yakichukuliwa tena bila hata ya sisi wenyewe kushirikishwa, yapimwe na kugawanywa vipande vipande kisha viizwe kwa matajiri, tutatetea haki yetu hata kama wakituletea FFU watupige mabomu,” alisema Mwandetele.
 
Naye Timoth Kaswaga alisema kuwa Taarifa walizozipata ni kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe tayari imekopa fedha benki na sasa inahitaji kuchukua ardhi yao iuzwe kwa ajili ya kulipa deni hilo.
 
Akizungumza na wananchi hao, Mwenyekiti wa Mujata, Chief Soja Masoko alisema kuwa kosa la Halmashauri ni kutowashirikisha wananchi katika mipango yake, hali ambayo inasababisha migogoro isiyokuwa ya lazima kwenye jamii.
 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispine Meela, akijibu tuhuma hizo, alikiri kuwepo kwa mpango huo na kukana yeye kuwa na maslahi ya aina yoyote na mpango huo.
 
Alisema baada ya Serikali kukaa, ikaona mji wa Tukuyu hauwezi kuendelea zaidi kutokana na asababu za kijiografia, na ndipo ilipoamuliwa kuwa Kata ya Kyimo iendelezwe na kuwa sehemu ya mji ndogo wa Tukuyu.
 
Alisema zaidi ya hekta 5000 zinahitajika kwa ajili ya kupimwa na kuendelezwa kwa kujengwa kituo kikuu cha mabasi, viwanda, makazi na uwekezaji wa aina mbalimbali.
Mwisho.

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top