Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
watuhumiwa wa vurugu hizo wakifikishwa mahakamani.


Na,Bosco Nyambege,Tunduma





Jeshi la polisi mkoani Mbeya, limefanikiwa kurejesha hali ya utulivu kufuatia vurugu zilizoibuka mapema leo asubuhi katika Mamlaka ya mji mdogo wa Tunduma na jeshi hilo kulazimika kutumia nguvu, huku watu 26 akiwemo Diwani wa kata hiyo Frank Mwakajoka kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za uchechezi.




Chanzo cha tukio hilo ni kugombea eneo  moja la wazi lililopo Sogea, linalodaiwa kumilikiwa Chama Cha Mapinduzi kata hiyo, ambapo wananchi wanahitaji kujenga zahanati huku CCM wakitaka kulitumia eneo hilo kwa matumizi mengine.




Habari zimeeleza kwamba, ujenzi wa zahanati hiyo ulianza wiki iliyopita ambapo baada ya kazi hiyo kuanza CCM walikwenda kupinga katika Baraza la kata ambalo liliwapo ushindi ccm, ambapo wananchi hao walikata rufaa baraza la ardhi la wilaya ambako walitupilia mbali dai hilo ndipo wakaanza kujenga kwa nguvu.




Mwenyekiti wa kitongoji cha Sogea ambaye hajataja jina lake amesema wanachohitaji wananchi wa Tunduma ni maendeleo na si vurugu kama ambavyo imetokea.




Mkurugenzi Mtendaji wa mji wa Tunduma Juma Kitabuge akizungumza na Ilasi fm kwa njia ya simu amesema kumbukumbu zinaonesha kuwa kiwanja hicho kinamilikiwa na CCM.




Amesema hata hivyo ameagiza kwamba kwa kuwa eneo hilo limekuwa na mgogoro basi lisifanyiwe shughuli yoyote hadi pale suala la msingi litakapofanyiwa kazi.



Kitabuge ameongeza kuwa ofisi yake imeagiza kila mwananchi anapotaka kujenga jengo lolote hata kama ni kiwanja chake aihusishe ofisi ya ardhi ili aruhusiwe na kwamba wananchi nao hawakufuata taratibu ikiwa ni pamoja na Idara ya afya.




Kwa upande wao viongozi wa CCM hawakupatikana na kuwa ofisi zao zimefungwa ikidaiwa kuwa wapo ziarani vijijini.




Kwa upande wake katibu wa chadema wilaya ya Momba Godfrey Siame akizungumza na kituo hiki amesema amesikitishwa na tukio hilo na kusema kwani jambo lililokuwa likifanyika ni kwaajili ya jamii na si kama lilovyochukuliwa kuwa ni la kisiasa.




Kufuatia vurugu hizo watu 26 wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya mbozi akiwemo diwani wa kata ya Tunduma Frank mwakajoka(CHADEMA) na wamenyimwa dhamana hadi march 30 mwaka huu.




Imedaiwa mbele ya hakimu wa mahakama ya wilaya Names Chami na mwendesha mashitaka wa polisi Joel Mori kwamba washitakiwa kwa pamoja bila uhalali walifanya mkutano kinyume cha kifungu 74 na 75, shitaka lingine ni kufanya fujo na kuchoma matairi barabarani kinyume na kifungu 89 (1) B, Kuharibu mali kinyume cha kifungu 326 (1) na kushawishi watu kutenda kosa.


Mwisho.

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top