Mkurugenzi
wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Matutu Chacha
(aliyesimama) akizungumza wakati walipofanya ziara ya kujionea miradi ya
kilimo mkoani Simiyu.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Kilimo, Bibi Rosebud Kurwijila
(kulia) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (hayupo pichani) kuhusu
nafasi ya TADB katika kuwasaidia wakulima nchini.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Anthony Mtaka akizungumza na ugeni kutoka Benki
ya Kilimo (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi
kati ya uongozi wa Mkoa huo, wataalam wa kilimo, mifugo na ushirika na
Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Kilimo.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bw. Dome Malosha (kulia) akizungumza katika Kikao na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
Mmoja
wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Kilimo nchini, Bw. Joseph
Mutashubilwa (wapili kulia) akichangia hoja wakati wa walipomtembelea
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Anthony Mtaka (hayupo pichani).
Na Mwandishi wetu, Simiyu
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Anthony Mtaka ameiomba Benki ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania (TADB) kuuwezesha mkoa wa Simiyu katika kufanya
mapinduzi ya Kilimo kupitia miradi ya kimkakati inayotekelezwa mkoani
humo.
Bw.
Mtaka amesema mkoa wa Simiyu umejipanga kutumia fursa za mikopo nafuu
inayotolewa na TADB ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha
wakulima wanalima kisasa ili kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.
Bw.
Mtaka aliongeza kuwa Mkoa wa Simiyu uko tayari kufanya kazi na Benki ya
Kilimo kupitia vikundi vya uzalishaji, Halmashauri na Miradi mbalimbali
inayotekelezwa mkoani humo, ikiwa ni pamoja na miradi ya mfano ya
umwagiliaji ya Mwamanyili Wilayani Busega ulio katika hatua ya upembuzi
yakinifu na Mwasubuya wilayani Bariadi ambao uko katika hatua ya ujenzi
wa miundombinu ya umwagiliaji.
“Tungehitaji
kuwa Mkoa ambao kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo tungetengeneza
namna ambayo ingewasaidia wakulima na ikasaidia mikoa mingine kuja kuona
maendeleo ya kilimo ambayo ni matokeo ya Serikali kuwekeza katika
Benki ya Kilimo” amesema Mtaka.
"Sisi kama Mkoa tumejipanga, tumetoa Elimu ya utayari na
namna
ya utekelezaji wa shughuli zote kwa wataalam wetu pamoja na wananchi na
isitoshe tayari tumeshafanya utafiti na kuandaa mwongozo wa uwekezaji
ndani ya mkoa, hivyo tunawakaribisha kuwekeza,” aliongeza.
Aidha,
Bw.Mtaka ameongeza kuwa Mkoa wa Simiyu unatekeleza Sera ya Uchumi wa
Viwanda chini ya Kauli Mbiu ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja”
ambapo hadi sasa kuna kiwanda cha chaki na maziwa na miradi mingine
minne ya viwanda iko katika upembuzi yakinifu.
“Hivyo
Benki ya Kilimo inaweza kuwekeza katika miradi hii kwa kuwawezesha
wakulima na wafugaji kuzalisha malighafi ya Viwanda hivyo au kuwa mdau
katika viwanda hivyo,” aliomba.
Kwa
upande, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bibi Rosebud
Kurwijila alisema kuwa Benki ya Kilimo imejizatiti katika kuchangia kwa
kiasi kikubwa katika kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo
kwa wakulima wa Tanzania ili kusaidia upatikanaji wa fedha na sera
nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.
Bibi
Kurwijila alisema kuwa katika kutekeleza mkakati wa kuwafikia wakulima
wengi zaidi nchini TADB imejipanga kutoa huduma kupitia kongani mpya
nane (8) ili kuongeza tija kwa wakulima nchini.
Alizitaja
Kongani hizo kuwa ni pamoja na Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya
Kaskazini na Kanda ya Mashariki. Nyingine ni Kanda ya Magharibi, Kanda
ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kusini na Zanzibar.
“Kongani
ni njia ya kimkakati ya kijiografia yenye kujikita katika shughuli za
kilimo zinazohusiana, wasambazaji, na taasisi zinazohusishwa katika
kujenga usawa wa moja kwa moja miongoni mwa wadau, hivyo ili kukidhi
mahitaji ya wakulima nchini, benki ya kilimo itawafikia kupitia njia
hii,” alisema.
Naye
Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB Augustino Matutu Chacha
amesema wamefurahishwa na utayari wa Mkoa wa Simiyu juu ya kuwawezesha
wakulima na Benki hiyo iko tayari kutoa mikopo pia kwa wakulima wa zao
la pamba ambao wanazalisha zaidi ya asilimia 60 ya pamba yote nchini ili
izalishwe kwa wingi zaidi na katika ubora wa hali ya juu.
Bw.
Chacha amesema wataalam wa kilimo wa Mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na
wataalam wa benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) watakutana ili
kuona namna watakavyofanya kazi kwa pamoja ili mikopo itakayotolewa
iweze kuwa wa manufaa kwa wakulima na nchi kwa ujumla.
Aidha
amewaeleza Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuwa, Halmashauri zinaweza
kupatiwa mikopo ili ziweze kuendesha miradi ya kilimo itakayoweza kuwa
vyanzo vipya vya mapato kwa Halmashauri zao.
Post a Comment