Anaandika Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.
TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU)mkoani Kilimanjaro,imemtia
mbaroni Daktari wa Hospital ya rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi
akituhumiwa kudai na kupokea rushwa ya shilingi 150,000.
Daktari
huyo,Deogratias Godfrey Urio,alikamatwa jana katika mji mdogo wa Himo
kwenye baa maarufu ya Mombasa High Way baada ya kuwekewa mtego na
makachero wa takukuru mkoani Kilimanjaro.
Taarifa
iliyotolewa leo Alhamisi kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Takukuru mkoa
wa Kilimanjaro(RBC),Holle Makungu imesema kuwa kukamatwa kwa daktari
huyo kunatokana na malalamiko ya ndugu wa mgonjwa aliyekuwa akipigwa
dana dana kupatiwa huduma ya upasuaji katika hospital hiyo.
Makungu
ameeleza katika taarifa yake kuwa,mgonjwa huyo alikuwa akihitaji
kufanyiwa upasuaji wa uvimbe katika kizazi chake tangu oktoba mwaka huu
baada ya kufanyiwa vipimo kwenye hospital hiyo na kubainika kuwepo kwa
uvimbe.
Lakini
licha ya kubainika kuwepo na uvimbe huo,mgonjwa huyo hakuweza kupata
tiba haraka baada ya kuelezwa na daktari huyo kuwa hawezi kufanyiwa
upasuaji huo hadi hapo atakapotoa fedha hizo.
Makungu
ameeleza kuwa,baada ya taarifa hizo kuwafikia,mtego uliandaliwa na
daktari huyo aliweza kutiwa mbaroni jana Novemba 15 akiwa kwenye baa
hiyo ya Mombasa High Way.
“Tunaendelea
na uchunguzi wa tuhuma hizo na atafikishwa mahakamani mara tu uchunguzi
utakapokamilika,takukuru inatoa rai kwa madaktari na wauguzi katika
hospital ya Mawezi kuzingatia viapo vyao ili Mawenzi iwe hospital ya
kuigwa kwa huduma bora”,amesema makungu.
Mkuu
huyo wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro akahitimisha taarifa yake kwa
kuonya kuwa kwa wale wachache watakaoendelea kutozingatia viapo
vyao,watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria na pia kuwataka
waajiri wao wachukue hatua kali za kinidhamu dhidi ya watumishi hao .
Post a Comment