Na Rhoda James, DSM
Waziri wa Madini Angellah Kairuki mwishoni mwa wiki alikutana na Ujumbe
wa Benki ya Dunia jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufahamiana na
kuangalia hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa Miradi ya
Madini inayotekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali
Madini (SMMRP) unaofadhiliwa na Benki hiyo kwa kushirikiana na Serikali.
Pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho, Waziri
Kairuki aliitaka Benki ya Dunia kuona namna ya kuwaendeleza Wataalam
wa Sekta ya Madini ili kuwezesha uwepo wa Watalaam wa kutosha
hususan katika masuala ya Uthaminishaji wa Madini ya Almasi, tanzanite
na madini mengine ya vito na pia masuala ya uongezaji thamani madini
kwa ujumla.
Pia, alishauri umuhimu wa kuboreshwa kwa Mtandao wa Huduma za
Leseni kwa Njia ya Mtandao (Online Mining Cadastre) ikiwa ni pamoja na
kuunganisha mtandao huo na Mamlaka nyingine ikiwemo Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ili taarifa
zote zinazohusu madini na mapato yatokanayo na madini ziweze
kupatikana kupitia mtandao huo.
Vilevile, aliishauri Benki hiyo kuhusu uuzwaji wa Madini ya Almas kwa njia
ya Mnada kama vile inavyofanyika kwa Madini ya Tanzanite, lengo likiwa ni
kuwezesha Serikali kunufaika na madini hayo.
Aliongeza kuwa, baada ya Serikali ya Tanzania kupitisha Marekebisho ya
Sheria ya Madini kupitia Sheria ijulikanayo kama (The written laws
(Miscellaneous Amendements) Act, 2017), alisema kuwa, baadhi ya
wawekezaji wameonesha wasiwasi kuhusu marekebisho hayo.
Hivyo, Waziri Kairuki amewataka wawekezaji kutokuwa na hofu kwani
mabadiliko hayo yanalenga kuhakikisha kuwa Serikali inanufaika ipasavyo
kutokana na rasilimali zake za madini. Aidha, alisema kwamba, nia ya
Serikali kuhusu kuvutia wawekezaji iko palepale ilimradi wazingatie Sheria
na taratibu.
Vilevile, Waziri Kairuki alieleza kwamba, ni vema Benki ya Dunia ikaangalia
namna bora ya kuhakikisha madini yote ya Tanzanite yanayouzwa nje ya
nchi yanakuwa na Hati ya Uhalisia inayoonyesha chanzo cha madini hayo
suala ambalo litawezesha Taifa kupata mapato stahiki kutokana na
rasilimali hiyo.
Vievile, Waziri Kairuki alizungumzia suala la udhibiti wa utoroshaji madini
na kusisitiza kuhusu kuwepo na namna bora ya kuzuia utoroshwaji wa
madini ya Tanzanite ikiwemo kujulikana kwa idadi ya wachimbaji wadogo,
wa kati, kiasi kinachopatikana na mahali madini hayo yanapouzwa.
Pia, Waziri Kairuki aliishukuru Benki ya Dunia kutokana na ushirikiano
ambao umekuwepo baina ya Serikali kwa kipindi chote na kueleza kuwa,
Serikali iko tayari kutekeleza miradi husika kikamilifu kwa lengo la kukuza
uchumi wa nchi.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila aliiomba
Benki ya Dunia kuleta Wataalam wa madini nchini ili waweze kutoa
mafunzo katika vituo vya Madini nchini ikiwemo Chuo cha Madini Dodoma
(MRI) na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) ili kuzalisha wataalam zaidi
katika Sekta hiyo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Tanzania Mhandisi Benjamin
Mchwampaka alisema kuwa, tayari Serikali imefanya jitihada kadhaa za
kuanzisha mfumo wa utoaji wa leseni kwa njia ya Mtandao. Aliongeza
kuwa, kinachotakiwa sasa ni kuimarisha zaidi mfumo huo ili taarifa zote
zinazohitajika na umma zinazohusu madini na mapato ya kodi na mrabaha
ziweze kupatikana kwa urahisi na kwa uhakika.
Aidha, Kamishna Mchwampaka aliiomba Benki ya Dunia kukijengea uwezo
zaidi Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kilichopo jijini Arusha ili kiweze
kutoa mafunzo ya Utambuzi wa madini na Uongezaji thamani kwa viwango
vya Kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bella Bird
alisema zipo fursa nyingi kwa Sekta ya madini na hivyo kuiomba Wizara ya
Madini kuhakikisha kuwa inatumia fedha zilizopo katika miradi husika na
kwa wakati.
Naye, Mwakilishi Mwandamizi Mradi kutoka Benki ya Dunia ambaye pia ni
Mtaalamu wa Madini kutoka Idara ya Nishati Endelevu nchini Merekani,
Mamadou Barry, alisema kuwa, Wizara ya Madini ihakikishe kuwa
inakamilisha ujenzi wa Kituo cha Madini kinachotarajiwa kujengwa eneo la
Mererani kwa wakati ili kuwezesha minada ya madini na maonesho ya
madini kufanyika kwenye kituo hicho, na hivyo kudhibiti utoroshwaji wa
madini.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Masula ya Madini kutoka benki hiyo
Sheila Khama aliishauri Serikali ya Tanzania kuona namna ya kushirikiana
na nchi nyingine kama Afrika Kusini hususan kwenye Mikutano ya
Uwekezaji madini ya Indaba ili kuendelea kuwavutia wawekezaji.
Aidha, alishauri Tanzania kujifunza kutoka nchi ya Ethiopia kuhusu namna
ya kudhibiti Wachimbaji Wadogo wa madini ya dhahabu kwa kuwa, nchi
hiyo unao mfumo bora Barani Afrika.
Pia, alisisitiza kuhusu umuhimu wa ushirikishwaji wa wanawake katika
shughuli za madini nchini.
Post a Comment